Rais Dkt.Mwinyi apokea pongezi za Mtawala wa Ras Al Khaimah

Salaam za pongezi zimendelea kutolewa na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kufuatia ushindi mkubwa wa Urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alioupata, Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni hapa nchini, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi.
Salamu za pongezi za hivi karibuni zimetolewa na Mtawala wa Ras Al Khaimah, Sheikh Saud bin Saqr Al- Qasimi. Katika salamu hizo Sheikh Saud bin Saqr Al-Qasimi amempongeza Rais Dkt. Rais Hussein Ali Mwinyi kwa ushindi huo mkubwa alioupata katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu 2020.

Kutokana na ushindi huo mkubwa alioupata Rais Dkt. Hussein, Sheikh Saud bin Saqr Al-Qasimi ameuelezea kuwa ni wa mafanikio makubwa yanayotokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea maendeleo wananchi wake wote.

Hivyo, Sheikh A-Qasimi amemuahidi Rais Dk. Mwinyi kwamba Ras Al Khaimah itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kwa manufaa ya pande zote mbili.

Nae Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwa upande wake ametoa shukurani zake za dhati baada ya kupokea salamu hizo kutoka kwa kiongozi huyo wa Rais Al Khaimah na kueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wake inazithamini na itaendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo.

Wakati huo huo, Rais Dkt. Hussein Mwinyi amempongeza kiongozi wa Oman Sultan Haitham Bin Tariq Al Said pamoja na wananchi wake kwa kusherehekea siku ya Uhuru wa Taifa hilo.

Aidha, katika salamu hizo Rais Dkt. Hussein amemuhakikishia kiongozi huyo wa Oman kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Oman sambamba na kuimarisha udugu uliopo kati ya wananchi wa Oman na wananchi wa Zanzibar.

Sambamba na hayo, salamu hizo zilieleza kuwa siku hii adhimu inaendelea kutoa nafasi zaidi ya mashirikiano kati ya pande mbili hizo pamoja na kupongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Oman katika kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimtakia heri, mafanikio, afya njema na maisha marefu kiongozi huyo wa Oman pamoja na wananchi wake wote sambamba na kukuza na kudumisha amani na maendeleo yaliopatikana nchini humo.

Oman ilipata uhuru wake kutoka ukoloni wa Kireno mnamo Novemba 18, mwaka 1660 chini ya kiongozi na muasisi wa Taifa hilo Iman Sultan Bin Saif Bin Malik Al Yarubi ambaye alisimamia kung’oka kwa koloni hilo kutoka nchini Oman pamoja na bandari zote za nchi hiyo zilizokuwa chini ya Utawala wa Kireno.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news