Rais Dkt.Mwinyi:Uchaguzi umekwisha,sasa ni kudumisha amani na kuilinda

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwiyi amesema kuwa uchaguzi umekwisha na umemalizika kwa salama na kilichobaki hivi sasa ni kuendelea kuidumisha na kuilinda amani iliyopo nchini,anaripoti Maalum Mwandishi Diramakini.
Alhaj Dkt. Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo Novemba 6,2020 mara baada ya sala ya Ijumaa katika Masjid Nunge jijini Dodoma wakati alipokuwa akiwasalimia Waislamu msikitini hapo mara baada ya kumalizika sala hiyo ya Ijumaa.

Katika salamu zake hizo, Alhaj Dkt. Hussein amewataka wananchi wote kuendelea kuidumisha na kuilinda amani kwani bila ya amani hakuna kitu kinachoweza kufanyika.

Ameongeza kuwa, katika hatua iliyopo hivi sasa ni muhimu amani iwe kitu cha mwanzo na kusisitiza kwamba mustakabali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unategemea amani kwa kiasi kikubwa.

Ameeleza kwamba, mara zote binadamu hajui umuhimu wa kitu hadi pale kinapomuondoka akimaanisha haja ya kuilinda na kuidumisha amani iliyopo hivi sasa ili isipotee huku akitolea mfano wa mwanaandamu anapokuwa na afya na pale anapoikosa.
Rais Dkt. Hussein Mwinyi amesisitiza kwamba, amani haijaribiki hivyo, alikemea viashiria vidogo vidogo vya kuvuruga amani iliyopo na kuwataka wananchi kuidumisha amani iliyopo na kutovipa nafasi viashiria hivyo.

Akitolea mfano wa baadhi ya nchi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu kama vile Yemen, Somalia, Syria na Iraq ambako amani imeondoka hivi sasa na kupelekea wananchi wake kutoishi vizuri pamoja na kukosa hata muda wa kufanya ibada.

Alhaj Dkt. Hussein Mwinyi ametoa shukurani kwa waumini wa Msikiti huo kwa kumuombea dua kwa wingi wakati wa mchakato wa kampeni za uchaguzi ambapo Mwenyezi Mungu amezikubali dua zao hizo.

Akitoa shukurani hizo, Alhaj Dkt. Hussein amesema kwamba, awamu ya kwanza ya kugombea nafasi ya uongozi imeshafanyika na Allah ameshaleta rehema za ushindi na lilolobaki hivi sasa ni kuwatumikia wananchi.

Hivyo, amewataka waumini hao waendelee kumuombea dua ili aweze kuwahudumia wananchi kwa haki, upendo, umoja na mshikamano mkubwa.

Sambamba na hayo, Alhaj Dkt. Hussein Mwinyi amewaeleza waumini hao kwamba hana cha kuwalipa ila ataendelea kuwaombea dua kwa Mwenyezi Mungu na kueleza furaha yake kwa kupata fursa hiyo ya kutoa salamu msikitini hapo huku akieleza kwamba historia zinaonesha kwamba Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi alikuwa akipewa fursa ya kusalisha msikitini hapo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news