Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameendelea kupongezwa na marais, viongozi, taasisi, mashirika na wananchi kutoka pande zote za Dunia huku wakimhakikishia ushirikiano wa hali ya juu kwa ajili ya kufanikisha ndoto yake ya kuivusha Tanzania kutoka uchumi wa Kati hadi wa juu, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Rais wa Zambia, Mheshimiwa Edgar Lungu ambaye amesisitiza kuwa, ushindi wa kishindo wa Dkt. Magufuli umepokewa kwa shangwe na wananchi wote wa Zambia, hivyo wataendelea kushirikiana bega kwa bega ili wananchi wa pande zote waendelee kunufaika na mahusiano mema ya pande zote katika nyanja mbalimbali.
"Pongezi zangu nyingi zimuendee kaka yangu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupewa dhamana tena, baada ya ushindi wa kishindo ulioupata mwishoni mwa wiki kupitia Uchaguzi Mkuu.
"Zambia inakuhakikishia ushirikiano mkubwa ikiwa ni mwendelezo wa kudumisha uhusiano mwema kwetu. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Zambia,"ameeleza Rais Edgar Lungu wa Zambia.
Rais Dkt. John Magufuli aliapishwa Novemba 5, 2020 jijini Dodoma kufuatia ushindi wa kihistoria alioupata kupitia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020 kwa kupata asilimia 84.4 ya kura ambazo ni kiwango cha juu zaidi.