Rais Magufuli awashukuru Wakristo kwa kuanzisha harambee ujenzi wa Msikiti

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. John Pombe Magufuli amewashukuru Waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Ikulu-Chamwino Mkoani Dodoma kwa kuanzisha harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti wa Chamwino ambao umekamilika na kuanza kutumika, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Mheshimiwa Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli ametoa shukrani hizo katika Misa Takatifu ya Jumapili ya 32 ya Mwaka “A” iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Paul Mapalala.

Amewashukuru Waumini wa Madhehebu mengine ya Dini waliojitokeza kuchangia ujenzi wa Msikiti huo pamoja na Kanisa la Bikira Maria Imakulata Ikulu-Chamwino ambalo ujenzi wake ulifanyika kabla, na amebainisha kuwa kitendo hicho kinadhihirisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati walionao Watanzania.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ambaye leo Novemba 8, 2020 amesali Ibada ya kwanza ya Jumapili tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili amewashukuru Waumini wa Madhehebu yote ya Dini kwa Sala na Dua zao za kuombea mchakato wa uchaguzi mkuu tangu wakati wa kampeni hadi kuapishwa kwake na amesisitiza kuwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais ni ushindi wa Watanzania wote.

Amewaomba viongozi wa Dini na Watanzania wote kuendelea kuliombea Taifa, na kuiombea Serikali anayoiongoza ili itekeleze ahadi zilizomo katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020/25 zilizolenga kujenga uchumi imara na ustawi wa jamii.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akishukuru baada ya kukabidhi michango kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya iliyotokana na harambee kuchangia ujenzi wa Msikiti wa Chamwino wakati wa Misa Takatifu ya Dominika ya 21 ya Mwaka “A” ambapo pia alizindua Kanisa, Nyumba ya Mapadres na Grotto ya Parokia ya Bikira Maria Imakulata Ikulu Chamwino Jumapili ya Agosti 23,. 2020. (MAKTABA).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news