Rais mteule wa Zanzibar, Dkt.Hussein Mwinyi anatarajiwa kuapishwa kesho Novemba 2, 2020 katika Uwanja wa Amani Abeid Karume uliopo Unguja jijini Zanzibar, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Katika hafla hiyo ya kuapishwa wageni mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria akiwemo Rais Mteule wa Tanzania ambaye ni Rais anayemaliza mhula wake wa kwanza wa Urais, Dkt.John Magufuli na Rais wa Zanzibar anayemaliza muda wake, Dkt. Ali Mohamed Shein.
Sambamba na wageni mbalimbali kutoka Namibia, Msumbiji, Uganda, Ghana, Kenya, China, Moroco, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui mjini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Abdulah Juma Sadala amesema, mabalozi zaidi ya 26 wa ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki katika hafla hiyo.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt.Abdulla Juma Mabodi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya maandalizi ya sherehe za kumuapisha Rais mteule wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi.
Amesema, wageni wengine wanaotarajiwa kushiriki katika sherehe hizo ni pamoja na vyama rafiki vya siasa kutoka nchi mbalimbali pia amewataka wananchi mbalimbali wa Zanzibar na nje ya Zanzibar kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Amani kushuhudia kuapishwa kwa Rais wa Awamu ya Nane wa Zanzibar.
"Nawaombeni sana mje kwa wingi wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi mje kushuhudia kile ambachomlikiamua katika chumba cha kupigia kura Oktoba 28, mwaka huu. Maandalizi yote yamekamilika,"amesema Dkt.Mabodi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, Dkt. Juma Mohammed amewataka wananchi wajitokeze mapema ili kuondoa usumbufu wa kuchelewa kuingia katika uwanja huo.