Rais Donald Trump wa Marekani amedai kufanyiwa wizi katika
uchaguzi mkuu wa taifa hilo pasipo kuwa na ushaihidi wowote. Amesema wapinzani wake wa Chama cha Democratic wanafanya jaribio la
wizi katika uchaguzi huo ambao alidai yeye anaweza kushinda kwa urahisi dhidi ya Joe Biden, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Trump ameyasema hayo katika Ikulu ya Marekani na kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari akisisitiza kuwa, "Kama ukihesabu kura halali, nitashinda kwa wepesi. Lakini kama utahesabu kura zisizo halali, wanaweza kutuibia uchaguzi huu".Kwa sasa timu ya Trump imeanzisha madai katika mamlaka husika kwa lengo la kukabiliana na kile Rais Trump alichokiita ufisadi wa chama cha Democrat.
Katika baadhi ya nchi za Afrika ambazo uchaguzi umefanyika hivi karibuni na kukumbwa na utata wa matokeo kama Guinea, baadhi ya raia wameeleza kusikitishwa na Rais Trump kudai ushindi wakati hata hesabu ya kura ilikuwa inaonyesha kwamba alikuwa nyuma ya Joe Biden.
Mory Keita, ambaye ni raia wa Guinea amesema kwamba, Rais Trump anaonyesha mfano mbaya sana kwa nchi za Afrika ambazo bado ni changa kidemokrasia, huku Bachir Diallo akisema kuwa hatua ya Trump ni ya kuleta fedheha sana kwamba hayo ni mambo ambayo yanatarajiwa kutokea katika nchi yenye utawala mbovu sana na wala sio Marekani.
Kura zinaendelea kuhesabiwa katika uchaguzi wa Marekani, Joe Biden akiwa anaongoza kwa idadi ya kura, lakini hakuna mshindi amepatikana hadi sasa.