RC Kunenge awataka wananchi kufanya mazoezi, kuepuka ulaji usiofaa

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanafanya mazoezi na kuepuka ulaji usiofaa ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, saratani na kisukari ambayo yamekuwa chanzo cha vifo na usumbufu kwa wananchi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

RC Kunenge amesema hayo wakati wa ufunguzi wa wiki ya kitaifa ya kukabiliana na Magonjwa yasiyoambukiza iliyoanza leo Novemba 7 hadi 14, 2020 kwenye Viwanja Mnazi mmoja ambapo amesema katika wiki hiyo wananchi watapata fursa ya kupima magonjwa mbalimbali bure na kupatiwa ushauri wa kitaalamu.

Aidha, RC Kunenge amesema kwa kuwa, magonjwa hayo yanaweza kuzuilika ni vyema wananchi wakaanza kuchukuwa tahadhari mapema kwa kuhakikisha wanazingatia ulaji bora, kupunguza ulevi usiofaa,kupunguza uvutaji wa sigara na kuzingatia michezo.

Pamoja na hayo RC Kunenge amesema, upande wa Serikali itaendelea kutoa elimu ya kutosha ya namna bora ya kukabiliana na magonjwa hayo na kuendelea kuboresha na kuongeza miundombinu mbalimbali ya afya.

Ufunguzi wa maadhimisho hayo umehusisha watendaji kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, mashirika na asasi za kiraia na yameenda sambamba na matembezi pamoja na mechi za kirafiki kati ya timu ya Azam na ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na timu nyingine.

Kwa mujibu wa takwimu mbalimbali za kitabibu duniani, magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa yakichangia vifo vingi vya watu kutokana na jamii nyingi kutojua namna ya kujikinga au kukabiliana nayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news