Ruvuma waongoza tena kwa mazao ya chakula nchini

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme amewapongeza wakulima wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuongoza tena nchini katika uzalishaji wa mazao ya chakula.

Mndeme amesema, katika Mkoa wa Ruvuma  msimu wa mwaka 2019/2020 Mkoa wa Ruvuma umeongoza tena katika uzalishaji wa  mazao ya chakula na kuwa mkoa wa kwanza kitaifa.

“Msimu wa 2020/2021,mahitaji ya chakula katika Mkoa wa Ruvuma ni tani 338,889 ikilinganishwa na tani 1,430,474 za mazao ya chakula zilizovunwa hadi mwezi Juni,2020 na hivyo kuwa na ziada ya tani 1,091,585,"amesema.

 Amesema, jumla ya hekta 474,901 zililimwa katika msimu wa mwaka 2019/2020  na kuzalisha tani 1,346,220 na kwamba katika msimu wa mwaka 2019/2020 Mkoa wa Ruvuma ulilima hekta 268,008 zilizotoa mavuno ya tani 787,321 hii ni sawa na ongezeko la tani 50,628 na kuongoza kitaifa katika uzalishaji wa mazao ya chakula.

Mndeme amesema, mafanikio hayo yaliyopatikana kwa miaka miwili mfululizo yametokana na uwepo wa nguvu kazi ya kutosha na utayari wa wananchi kushiriki katika shughuli za uzalishaji ambapo hadi sasa Mkoa una  chakula cha kutosha na ziada.

“Mkoa una jumla ya hekta 4,007,746 za ardhi zinazofaa kwa kilimo, katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015 - 2020 Mkoa umeweza kuzalisha tani 8,547,816 za mazao hadi kufikia mwaka 2020,’’amesisitiza.

Hata hivyo, Mndeme ameyataja mahitaji ya chakula katika Mkoa wa Ruvuma kwa mwaka 2020 ni tani 469,172 ikilinganishwa na uzalishaji wa mazao ya chakula ni tani 1,346,220 na hivyo Mkoa una ziada ya chakula tani 877,048.

Kulingana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,zao la mahindi linaongoza kwa kulimwa kwenye maeneo mengi  hivyo kulifanya kuwa zao la chakula na biashara ambapo msimu wa kilimo wa mwaka 2019/20 Mkoa ulizalisha tani 787,321 katika hekta 268,008.

Amesema uzalishaji huo umechangiwa na matumizi ya zana bora za kilimo na matumizi ya pembejeo za Kilimo  kama mbolea na mbegu bora na kwamba matumizi ya mbolea yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka.

Takwimu zinaonesha kuwa, toka mwaka 2015 hadi kufikia 2020 mbolea iliyotumika katika Mkoa wa Ruvuma ni Jumla ya tani 167,758.5 ambapo Mkuu wa Mkoa amesema kiasi hicho cha mbolea kimepatikana kutokana na Serikali kuandaa mazingira mazuri ya uingizaji wa mbolea nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news