Hivi karibuni Rais John Pombe Magufuli amezindua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia ushindi wa kishindo alioupata katika uchaguzi wa mwezi Oktoba, ambapo alichaguliwa kuiongoza nchi kwa kipindi kingine cha miaka mitano,anaripoti Jovina Bujulu (MAELEZO).
Katika hotuba yake ya uzinduzi, Rais Magufuli alionyesha dira, falsafa, mwelekeo na vipaumbele vya nchi katika kipindi cha uongozi wake wa miaka mitano. Pamoja na mengi aliyozungumzia , Rais aliahidi kuboresha vitambulisho vya wajasiriamali ili waweze kutambulika rasmi na kuweza kupata mikopo katika taasisi za fedha hapa nchini.
Rais Magufuli alisema kuwa, kama alivyoahidi wakati wa kampeni kwamba katika kipindi cha uongozi wake wa miaka mitano ijayo, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa wajasiriamali wadogo, machinga, mama lishe, baba lishe waendesha boda boda na bajaji.
Tangu ilipoingia madarakani, Serikali ya Awamu ya Tano ilianza kuwatambua rasmi wajasiriamali wadogo nchini pote kwa kuwapatia vitambulisho ambavyo vilikuwa vinalipiwa shilingi 20,000 kwa mwaka. Utambuzi huo uliwapa uhuru wajasiriamali hao wadogo kufanya biashara zao bila kubugudhiwa na mtu au mamlaka yoyote hivyo kujiongezea kipato.Muonekano wa kitambulisho cha Mjasiriamali
Vitambulisho hivyo vya awali vilitolewa na Rais Magufuli mwaka 2018, ambapo jumla ya vitambulisho 670,000 vilitolewa na kuwawezesha wafanyabiashara ndogo ndogo kutambulika nchini na kuhakikisha wanafanya shughuli zao bila kusumbuliwa na kama ilivyokuwa awali ambapo walikuwa wanasumbuliwa sana na mamlaka mbalimbali za miji na halmashauri.
Katika utaratibu wa awali, kila mkoa ulipewa vitambulisho 25,000, ambapo kila mjasiriamali aliyekihitaji alikilipia na pesa ilipelekwa TRA na vilikuwa vinatolewa kwa hiari. Utaratibu huo ulimwezesha kila Mkuu wa Mkoa kukusanya shilingi milioni 500 ambazo ni mchango wa sekta hiyo ya wafanyabiashara.
“Miaka mitano iliyopita tulianzisha utaratibu wa kutoa vitambulisha maalum kwa wajasiriamali wetu wadogo, tunakusudia kuviboresha vitambulisho hivyo kwa kuweka picha na taarifa nyingine muhimu kama ilivyo kwenye vitambulisho vya Taifa (NIDA) na kwenye Hati za kusafiria(Pasipoti)”, alisema Rais Magufuli.
Kuboreshwa kwa vitambulisho hivyo kutakuwa ni fursa nyingine muhimu kwani wataweza kukua na kutajirika na kuondokana na dhana ya kuwa wafanyabiashara wadogo ambapo hii itawezekana kwa sababu wataweza kutambulika kwenye taasisi za fedha na kuweza kupata mikopo kwa ajili ya kukuza biashara.
Aidha, kutokana na maboresho hayo wajasiriamali hao wataweza kukuza mitaji yao kwa kuwa sasa watakuwa na uwezo wa kukopa na kuweza kupanua biashara zao nchi nzima. Hivyo ni wakati muafaka kwao kukuza na kupanua biashara zao kwa sababu ya uwezo wao wa kuongeza mtaji utakuwa umerahisishwa.
Endapo wajasiriamali hao wataitumia fursa hii ipasavyo mbali na kuweza kupata mikopo ya biashara , wataweza pia kupata mikopo mikubwa ambayo itawanasua katika umaskini ikiwa ni pamoja na kubadilisha biashara zao kutoka kuwa ndogo ndogo na kuwa za kati hadi za juu.
Vitambulisho hivyo pia vitawafanya wajiamini zaidi ikiwa ni pamoja nakuongeza bidii katika shughuli zao kwani sasa wataweza kukopesheka kutokana na kuwa na vitambulisho hivyo vilivyoboreshwa. Hivyo wafanya biashara hawana budi kuchangamkia fursa hii kwa kuhakikisha kuwa wanavipata pale vitakapokuwa vimeanza kulipiwa.
Kufuatia kauli ya Rais kuhusu kuboresha vitambulisho hivyo wajasiriamali wameonesha kufurahishwa na hatua hiyo na kusema kuwa sasa ni wakati wa kukuza mitaji yao na kuinuka kiuchumi. Mama Lishe, Mwajuma Salum wa soko la Mwananyamala amesema kuwa, “ Rais Magufuli kweli ni mkombozi wa wanyonge, miaka yake mitano ya mwanzo alitupatia vitambulisho na hivyo kutuwezesha kufanya biashara zetu kwa amani bila kusumbuliwa na mtu yeyote, sasa amesema ataboresha vitambulisho hivyo ili tuweze kukopesheka, Mungu amlinde”.
Naye muuza matunda katika eneo la Afrika Sana Sinza, Mary Zephania amesema, “ Vitambulisho vikiboreshwa na nikapata cha kwangu hatua ya kwanza nitakwenda kuomba mkopo ili nikuze mtaji wa biashara yangu ili ikiwezekana niweze kusafirisha matunda hata nje ya nchi”.
Baadhi ya wafanyabishara wadogo wadogo wa soko la Manzese wamesema kuwa wana imani na Serikali ya Rais Magufuli ambayo wakati wote ina dhamira ya kuwaondoa katika umaskini, maana tangu Rais aingie madarakani amekuwa akihimiza kuondolewa changamoto mbalimbali zinazowakabili wajasiriamali.
Tangu kuingia madarakani mwaka 2015, Rais Magufuli amechukua hatua mbalimbali za kuimarisha uchumi na kuwakomboa wananchi kutoka katika umaskini na kuwawezesha kufanya biashara bila kusumbuliwa ili kuwafanya wawe matajiri. Aidha katika hotuba yake kwa Bunge la 12, ameendelea kusema kuwa Serikali atakayoiunda itaendeleza jitihada za kukuza uchumi
Tags
Makala