Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella amepiga marufuku aina yoyote ya maandamano na mikusanyiko huku akiwataka wananchi kuendelea kujikita kwenye shughuli za kimaendeleo kwa maslahi mapana ya Taifa kutokana na kwamba uchaguzi umekwisha na walioshindwa wakubali matokeo, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Shigella ameyasema hayo wakati madereva wa pikipiki maarufu bodaboda walipokusanyika kwa ajili ya kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kuchaguliwa tena kuongoza Tanzania kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella akizungumza na madereva wa pikipiki maarufu bodaboda waliokusanyika kwa ajili ya kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kuchaguliwa tena kuongoza Tanzania kwa kipindi kingine cha miaka mitano, kushoto ni Katibu wa Kikundi cha Tanga One cha wilaya ya Tanga, Omari Ahmed.
Amesema kwamba, amepokea maandamano hayo ili atumie nafasi hiyo kuwatangazia wananchi kwamba Serikali hairuhusu mikusanyiko yoyote katika kipindi hiki ambacho uchaguzi umemalizika.
Hatua ya mkuu huyo wa mkoa kupiga marufuku maandamano au mikusanyiko yoyote imekuja kutokana na uwepo wa tetesi kwamba wafuasi wa baadhi ya vyama vya upinzani wanaandaa maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella kulia akiteta jambo na viongozi waendesha bodaboda wa kikundi cha Tanga One wakati akipokea maandamano yao waliokusanyika uwanja wa Lamore kwa ajili ya kumpongeza Rais Dkt.John Magufuli kwa kupata ushindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu.
Awali akisoma risala ya umoja wa waendesha bodaboda wa kikundi cha Tanga One cha wilaya ya Tanga iliyosomwa na Katibu wao, Omari Ahmed amesema wanampongeza Rais Dkt.John Magufuli kwa ushindi walioupata na kwamba wana matumaini kwamba sasa wana uhakika wa kufanya kazi zao kwa utulivu.
Amesema, wanampongeza kwa dhati Rais Magufuli kwa kuibuka na ushindi wa kishindo kwani walikuwa wanamuombea kila wakati katika mchakato huo wa kuwania nafasi hiyo.
“Pia tunapongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha amani ya Taifa inakuwa shwari wakati wote huu wa uchaguzi na umekwisha sasa tunaangalia maendeleo zaidi na kauli mbiu ya Rais Dkt.Magufuli ya hapa kazi tu,”amesema.
Pia amesema, wao bodaboda kwa niaba ya wenzao wana ombi kwa Rais, wanaomba aendelee kuwakumbuka watu wa Tanga huku wakiomba wakati akiapishwa waalikwe watu 10 wa bodaboda waende kushuhudia tukio hilo.
Tags
Habari