Siku moja baada ya kifo cha mwanakandanda Diego Maradona, ambaye alikuwa anajulikana sana duniani kama mmoja wa wachezaji mahiri kufariki dunia kwa mshtuko wa moyo, maombolezo yameanza huku salamu za rambirambi zikiendelea kumiminika kutoka kila kona ya Dunia, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Waombolezaji wakiwa wamekusanyika leo nje ya nyumba ya marehemu Diego Maradona mjini Buenos Aires, Argentina huku wakiwa wamechukua tahadhari kubwa dhidi ya virusi vya corona (COVID-19). Nyota huyo anakumbukwa kwa rekodi kubwa alizoziweka katika soka nchini mwake na Duniani kwa ujumla. (Picha na AP/Diramakini).
Diego Armando Maradona alizaliwa Octoba 30, 1960,alikuwa na umri wa miaka 60 hadi umauti unamfika hivi karibuni alikuwa na matatizo ya kiafya na kufanyiwa upasuaji baada ya damu kuganda kwenye ubongo wake wiki chache zilizopita. Alipata mshtuko wa moyo akiwa nyumbani mjini Buenos Aires siku ya Jumantano nchini Argentina.
Kufuatia kifo hicho Rais wa Argentina, Alberto Fernandez ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa huku nyota wa Kimataifa katika kandanda kutoka Brazil, Pele akiwa miongoni mwa watu waliokuwa wanaomboleza kifo cha Maradona.
“Kwa kweli kuna siku, tutacheza mpira pamoja tukiwa mbinguni,” amesema Pele katika taarifa yake fupi kwa shirika la habari la Reuters.
Moja ya mambo ambayo Maradona atakumbukwa katika historia ya soka ni pale alipokuwa nahodha wa timu ya Argentina katika kombe la dunia mwaka 1986, kabla ya kuingia katika matatizo na kuondolewa katika kombe la dunia mwaka 1994, kwa kupima na kukutwa alikuwa ametumia dawa zilizopigwa marufuku.
Miaka kadhaa ya matumizi ya dawa, kula kupita kiasi na pombe viliingilia kati umahiri wake katika kandanda, mwaka 2000 alikaribia kupoteza maisha kwa kutumia dawa za kulevya.
Mchezaji huyo wa Argentina, aliyefunga magoli 259 katika mechi 491 alizoshiriki alimshinda mpinzani wake wa Marekani Kusini katika kura ya maoni ya kuamua mchezaji wa karne ya 20 kabla ya Shirikisho la Mpira Duniani (FIFA) kubadilisha sheria za upigaji kura na wote wawili wakatunukiwa hadhi hiyo.
Mzaliwa huyo wa Tigre nchini Argentina ni baba wa watoto Diego Sinagra, Giannina Maradona, Dalma Maradona, Diego Fernando Maradona Ojeda, Jana Maradona.
Kumbukumbu zinaonesha kuwa, Maradona alionesha uwezo wa hali ya juu kutoka akiwa mtoto na kuwa chanzo cha timu ya vijana ya Los Cebollitas kuwa kidedea kwa kupata magoli 136 bila kufungwa na timu yoyote mbali na kujitokeza kwake kama mchezaji wa kimataifa akiwa na umri wa miaka 16 pekee na siku 120.
Akiwa mfupi na imara, futi tano na inchi tano pekee, uchezaji wake haukuwa wa kawaida. Wachambuzi wa soka wanasema, ujuzi wake, wepesi, maono, jinsi alivyodhibiti mpira, alivyopiga chenga na kupitisha mpira kwa wengine kwa sababu ya kukosa kasi na wakati mwingine hata kuwa na matatizo ya uzito wa kupita kiasi ni moja kati ya sababu ambazo zilimfanya kuwa mtu wa kipekee
Aidha, inatajwa alikuwa na kasi ya ajabu akiwa uwanjani karibu na mahasimu wake, lakini alikuwa na wakati mgumu kukwepa changamoto.Maradona alifunga magoli 34 kwa kushiriki mechi 91 kama mchezaji wa Argentina na yeye ndio chanzo cha nchi yake kuibuka na ushindi katika Kombe la Dunia mwaka 1986 nchini Mexico na kupata fursa kuingia fainali miaka minne baadaye.
Katika robo fainali ya mchezo wa awali kulijitokeza utata ambao kumbe baadaye ungekumba maisha yake.Mechi dhidi ya England ilikuwa na mkwaruzano uliopitiliza kidogo huku vita vya Falklands kati nchi hizo mbili vikiwa ndio vimetokeo miaka minne tu nyuma. Na kumbe hilo lingesababisha hali uwanjani kuzua wasiwasi zaidi.
Dakika 51 zikiwa zimekatika na hakuna timu iliyoona lango la mwingine, Maradona aliruka na mlinda lango wa timu pinzani Peter Shilton na kufunga kwa kupiga mpira hadi kwenye neti.
Baadaye alisema goli hilo lilitokana na "Maradona kuupiga mpira kwa kichwa kidogo na mkono wa Mungu". Dakika nne baadaye, alifunga kile ambacho kimekuwa kikitambuliwa kama 'goli bora la karne' - baada ya kuchukua mpira mwenyewe na kuanza mbio kwa kasi ya ajabu ambako kuliacha wachezaji kadhaa wakimfuata nyuma kabla ya kumzunguka Shilton na kufunga bao.
Maradona alivunja rekodi ya uhamisho mara mbili akiondoka timu ya vijana ya Boca Juniors mji wake wa nyumbani na kujiunga na timu ya Barcelona, Uhispani kwa kima cha pauni milioni 3 mwaka 1982 na kujiunga na klabu ya Italia ya Napoli miaka miwili baadaye kwa kima cha pauni milioni 5.
Aidha, waliompokea walikuwa ni zaidi ya mashabiki 80,000 waliomsubiri uwanja wa Stadio San Paolo alipowasili kwa helikopta. Maradona alichezea klabu bora katika taaluma yake nchini Italia akishangiliwa na wafuasi wake wakati huo akiwa kichocheo cha kupata mataji ya kwanza ya Ligi mwaka 1987 na 1990 na pia katika Kombe la UEFA mwaka 1989.
Sherehe ya kufurahia ushindi wa kwanza ilidumu kwa siku tano huku maelfu ya watu wakijitokeza lakini Maradona alionekana kuchoshwa na sherehe hizo.
"Huu ni mji mzuri, lakini napata shida, hata siwezi kupumua kwa amani. Nataka kuwa huru na kutembea. Mimi ni kijana kama mwingine yeyote yule,"Diego Maradon alikaririwa nyakati hizo.
Maradona, baada ya kushindwa bao 1-0 na Ujerumani mwaka wake wa mwisho Italia mwaka 1990, alikutwa na kashfa ya utumiaji wa dawa zilizopigwa marufuku mwaka uliofuata na kupigwa marafuku kucheza soka kwa miezi 15 baadaye alirejea tena kwenye ulimwengu wa soka katika Kombe la Dunia la mwaka 1994 nchni Marekani.