Serikali yatoa maagizo kwa viongozi Mamlaka za Serikali za Mitaa

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga amewaagiza wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanaanza maandalizi kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza hapo mwakani,anaripoti Angela Msimbira (OR-TAMISEMI).

Mhandisi Nyamhanga ametoa agizo hilo leo jijini Dodoma wakati wa kuelezea tathimini ya matokeo ya darasa la saba kwa mwaka 2020 ambapo ufaulu wake umekuwa asilimia 82.68.

Amesema viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri wakishirikiana na wadau wa elimu wanatakiwa kuhakikisha miundombinu, samani na kuweka mazingira mazuri ya kuwapokea wanafunzi wote watakaochanguliwa kuanza kidato cha kwanza Januari 2021. 

“Kwa sasa tuko katika mchakato wa kuchagua wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza januari 2021, hivyo viongozi waanze kuweka mazingira ya kuhakikisha wanafunzi wote waliochanguliwa wanasajiliwa shuleni bila vikwazo vyovyote ili kutekeleza sera ya elimumsingi bila malipo.”Amesisitiza Nyamhanga. 

Amewakumbusha wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi watakaochanguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanaandikishwa na kuhudhuria kikamilifu darasani.

Aidha, Mhandisi Nyamhanga ametumia fursa hiyo kuwakumbusha viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri kukamilisha maandalizi yote yanayotakiwa kwa ajili ya uandikishaji wa wanafunzi wa shule za awali na darasa la kwanza watakaoanza masomo Januari 2021.

Hata hivyo, Mhandisi Nyamhanga ameipongeza Mikoa mitatu ya Simiyu, Mara na Lindi ambayo wastani wa ufaulu umekuwa ukiongezeka kila mwaka kwa miaka mitatu mfululizo matokeo ya Kumaliza Elimu ya Msingi.

Mkoa wa Simiyu ufaulu umekuwa ukiongeza kutoka wastani wa asilimia 70.65 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 91.98, huku Mara ikiongeza wastani wa ufaulu kwa asilimia 63.68 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 77.98 mwaka 2020 huku Lindi imeongeka kutoka asilimia 68.71 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 82.25.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news