Siri ya Lema kuichafua Tanzania yafichuka, 'atimuliwa Kenya'

Mpango wa aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema kutaka kuichafua Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uga wa Kimataifa umekwama na muda si mrefu anarejeshwa nchini baada ya kuwekwa rumande mjini Kajiado nchini Kenya, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Sinema ya Godbless Lema inakwenda sambamba na ya Tundu Lissu ambaye amejificha Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini, huku hii ya Lema inakuja siku moja kabla ya kuapishwa Mbunge Mteule wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu alimshinda kwa kura 82,480 huku Lema akiambulia kura 46,489.

Matokeo hayo ya kura ni kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo inaonyesha wazi kwa, Gambo alipata karibu mara mbili ya kura za Lema, ambapo Gambo anatarajiwa kuapishwa mapema wiki hii bungeni jijini Dodoma.
Novemba 8, 2020 Lema akiwa na mkewe Neema wakiwemo watoto wao watatu Brilliance, Terrence na Allbless wamekamatwa na Polisi katika Kaunti ya Kajiando nchini Kenya baada kuvuka mpaka wa Namanga bila kufuata taratibu za Kimataifa ikiwemo kuwa na hati ya kusafiria.

Lema amekaririwa na moja ya chombo cha habari nchini Kenya akisema kuwa, ameacha kila kitu nyumbani.

Kwa madai kuwa, vitu hivyo havina umuhimu kwa sasa. "Muhimu ni usalama wangu na usalama wa familia yangu. Nipo na wanangu Allbless, Brilliance na Terrence. Sijui kesho itakuja na nini. Kwa sasa natafuta hifadhi,"alikaririwa Godbless Lema ambaye awali alidanganya mpakani kuwa anaenda kuwatafutia watoto wake shule nchini Kenya.
 
Punde, Afisa wa awali ambaye alizungumza na Mwandishi Diramakini amesema kuwa, Godbless Lema anarejeshwa nchini Tanzania muda si mrefu.

"Sisi huku hatufanyi mambo kwa mitandao, hii tabia ya kutafuta sympathy kwa social media, ndio upate macomments na likes mingi ikomee huko huko kwao, na si hapa tafadhali. Tunafanya kazi kwa kufuata taratibu na sheria, hivyo Lema Godbless amekuja huku kwetu kwa kuvamia, nasi bila shaka tutamrejesha masaa machache, hii ni tabia mbovu, hauwezi kimbia pahali penye amani unadanganya eti unaenda kutafuta usalama huku,"amefafanua Afisa huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news