Ubunge wa Mdee, wenzake 18 wadaiwa kufikia kikomo

Siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwavua uanachama na nafasi zote za uongozi wabunge 19 wa Viti Maalum, Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa amesema kwa mujibu wa katiba mpaka sasa wabunge hao hawana tena sifa ya ubunge, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Wabunge hao ni Halima Mdee,Asia Mohamed, Felista Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Simon, Anatropia Theonest,Salome Makamba, Conchester Lwamraza, Grace Tendega, Ester Matiko,Secilia Pareso,Ester Bulaya, Agnes Kaiza, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga na Tunza Malapo.

Mzee Msekwa amesema, wabunge hao pia hawana tena sifa za kuwa wabunge kwa kuwa hawana chama kilichowapeleka bungeni na hata wakihamia chama kingine hawawezi kupata nafasi hizo, labda mpaka uchaguzi ujao (2025).

Kauli hiyo ameitoa hii leo Novemba 28, 2020, wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, ilipotaka kufahamu kama sheria na taratibu za Bunge zinaruhusu mbunge asiyekuwa na chama kuendelea kushika nafasi hiyo, hii ni baada ya wabunge hao kufukuzwa uanachama na chama chao cha CHADEMA usiku wa kuamkia leo.

"Siyo sheria ya Bunge hiyo ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inasema kuwa mbunge akiacha kuwa mwanachama wa chama kilichompeleka Bungeni na ubunge wake unakwisha, Spika Ndugai, hapati ugumu wowote wanapoondolewa yeye ni mpokeaji tu, ni kama mganga wa hospitali anapokea wagonjwa akiwatibu wanaondoka na wakifa wanaondoka na hakuna anayeweza kuvunja katiba,"amesema Spika Mstaafu Mzee Pius Msekwa.

Jana usiku, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe alitangaza kuwa, Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi Novemba 27,2020 imeazimia kuwavua uanachama wanachama na viongozi hao.

"Wamekinajisi chama na wamekataa kuja kwenye Kamati Kuu. Chama chetu hakijateua wabunge wa Viti Maalum tunaona tu watu wetu wanaapishwa na hatuna taarifa, hatujapeleka majina, fomu za tume zipo ofisini, mama zetu hawa, dada zetu hawajajaza fomu, ila tunaona tu wanaapishwa. Kamati Kuu imewavua uongozi wale wote ambao walikuwa viongozi kwenye mabaraza kati ya hao dada zetu 19 sitaki kupoteza muda kuwataja majina, kwa hiyo kuanzia sasa hawapaswi kushughulika na lolote kama viongozi na tumeelekeza nafasi zao zizibwe haraka,"amefafanua Freeman Mbowe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news