Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto duniani (UNICEF) limempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuchaguliwa kwa kishindo na wananchi katika kuiongoza Zanzibar katika uchaguzi mkuu uliopita mwaka huu, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Kupitia salamu za pongezi shirika hilo limempongeza Rais Dkt. Mwinyi na
kueleza kwamba, ushindi wake huo utaimarisha zaidi uhusiano na
ushirikiano uliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na shirika
hilo.Salamu hizo zimetolewa na UNICEF kupitia Mwakilishi wake hapa Tanzania, Bi Shalini Bahuguma akieleza kwamba shirika hilo limeanza kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa muda mrefu katika kuwahudumia, watoto, vijana na wanawake.
Salamu hizo pia, zimeeleza kwamba shirika hilo litaendelea kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa karibu zaidi pamoja na kuendelea kuwaunga mkono wanawake na watoto wa Zanzibar.
Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi kwa upande wake ametoa shukurani kwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa linalowahudumia watoto duniani (UNICEF) kwa salamu hizo za pongezi na kueleza kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itaendelea kushirikiana na shirika hilo.
Katika salamu hizo za pongezi Rais Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa, Serikali inatambua na inathamini juhudi kubwa zinazochukuliwa na shirika hilo katika kuhakikisha watoto, vijana pamoja na wanawake wanapata haki zao za msingi.
Hivyo, Rais Dkt. Mwinyi amelihakikishia shirika hilo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itashirikiana kikamilifu na Shirika hilo katika kutatua changamoto zinazowakabili watoto sambamba na kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo.
Wakati huo huo, kwa niaba ya Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Makamu Mwenyekiti wa chuo hicho, Profesa William Anangisye amempongeza kwa dhati Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Salamu hizo zimeeleza kwamba ushindi wa Rais Dkt. Hussein Mwinyi unadhihirisha imani kubwa waliyonayo kwake wananchi wa Zanzibar kuwa atawaletea maendeleo makubwa na kutatua kero zinazowakabili kama alivyoahidi katika Kampeni za uchaguzi.
“Sisi Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam tumeupokea ushindi wako kwa moyo mkunjufu na kwa furaha kubwa. Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam ni moja ya taasisi za umma na inahudumia Watanzania wote.
"Aidha, Chuo Kikuu kimekuwa kikipata ushirikiano mkubwa kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,"ilieleza sehemu ya salamu hizo za pongezi.
Aidha, salamu hizo zilieleza kwamba chuo hicho hivi sasa kimeendelea kuimarisha taaluma na kimeimarisha Taasisi ya Sayansi za Bahari iliyopo Zanzibar ambapo pia, kuanzia mwaka wa masomo uliopita chuo hicho kilianzisha Shahada ya awali ya masuala ya Sayansi Baharini.
Sambamba na hayo, katika salamu hizo zilizotolewa na Profesa Anangisye zilieleza kwamba Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam kimejipanga kuchangia kiasi kikubwa katika kukuza Uchumi wa Buluu ambayo ilikuwa moja ya ahadi alizozitoa Rais Dk. Hussein Mwinyi katika Kampeni za uchaguzi za mwaka huu 2020.
Nae Ras Dkt. Hussein Mwinyi kwa upande wake alieleza jinsi alivyopokea salamu hizo za pongezi kwa furaha kubwa na kutoa shukurani zake za dhati kwa Profesa Anangisye na kwa Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam kwa kuthamini ushindi wake alioupata kutoka na uchaguzi Mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita.
Kadhalika, Rais Dk. Hussein Mwinyi alieleza kufarajika kwake kutokana na taarifa ya maendeleo makubwa ya Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam na azma ya Chuo hicho katika kuchangia kukuza Uchumi wa Bahari ambayo imeanza kujitokeza katika jitihada za kuimarisha Taasisi ya Sayansi za Bahari iliyopo Zanzibar.
Pamoja na hayo, Rais Dkt. Hussein Mwinyi alikipongeza Chuo hicho kwa kuonesha utayari wake katika kumpa ushirikiano utakaohitajika kwa ajili ya ustawi wa Taifa na kwa mnasaba huo anawahimiza kuandaa programu nzuri zaidi zinazokwenda na mahitaji ya sasa ya kiuchumi hasa katika uchumi wa Buluu, Madini na Viwanda ili kuziongezea thamani rasilimali zitokanazo na bahari, maziwa, mito na migodi.
Tags
Zanzibar