Maandalizi ya hafla ya kumwapisha Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli itakayofanyika Novemba 5, 2020 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma yamekamilika, wanaripoti Eleuteri Mangi na Jonas Kamaleki (MAELEZO), Dodoma.
Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 4,2020 jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi mara baada ya viongozi kukagua uwanja huo utakaotumika kwa hafla ya kitaifa ya kumwapisha Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwa mara ya kwanza kiapo cha Rais kinafanyika hapa Dodoma, ni jambo la kihistoria ambalo wananchi wanapaswa kulifahamu. Uwanja wa Jamhuri Dodoma upo tayari kwa ajili ya shughuli ya kesho maandalizi yote yamekamilika”, amesema Dkt. Abbasi.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dodoma kuhusiana na maandalizi ya hafla ya kumuapisha Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, itakayofanyika Novemba 5, 2020 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Katika kufanikisha shughuli hiyo, Dkt Abbasi amesema kuwa nchi yetu itapokea ugeni mkubwa ambao utashiriki kwenye kiapo cha Mhe. Rais Mteule, Dkt. Magufuli ambapo watakuwepo viongozi wakuu wa nchi au wawakilishi wa wakuu hao wapatao 20 ambao wamethibitisha kushiriki.
Marais ambao wamethibitisha kuwepo kwenye hafla hiyo ni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa Comoro Azali Assoumani na Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa.
Viongozi wengine ambao wamethibitisha kushiriki ni ni pamoja na Mawaziri Wakuu, Makamu wa Rais wa nchi mbalimbali za Afrika, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ambaye atamwakilisha Mfalme wa huko.
Aidha, Rais Mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo na Nabii TB Joshua watashiriki pamoja na mabalozi 83 wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini
Katika hafla hiyo watashiriki pia viongozi waandamizi wa Serikali wakiwemo Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, viongozi wa taasisi za umma na binafsi, viongozi wa siasa, viongozi wa dini pamoja na Mawaziri na Manaibu Mawaziri wanaomaliza muda wao.
Fauka ya hayo, Dkt. Abbasi amesema kuwa viongozi wote walioalikwa ambao wana kadi za mwaliko, magari yao yatapaki Bustani ya Chinangali karibu na uwanja wa ndege wa Dodoma ambapo watapanda mabasi kuwapeleka eneo la tukio.
Hafla hiyo itakuwa na sehemu mbili ambapo kutakuwa na gwaride la kiapo litaongozwa na majeshi ya ulinzi na usalama na sehemu ya burudani ambayo itawashirikisha wasanii mbalimbali nchini ikizingatiwa Tanzania ni nchi ya amani na ni siku ya furaha.
Tags
Habari