Umoja wa Vyama vya Upinzani Zanzibar umesema umekubaliana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28,2020 na unamuunga mkono Rais wa Awamu ya Nane, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na wapo tayari kushirikiana katika kuijenga Zanzibar mpya.
Akizungumza kwa niaba ya vyama tisa vya siasa, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir katika ukumbi wa Wizara ya Habari Kikwajuni jijini Zanzibar amesema, uchaguzi uliofanyika ulikuwa ni wa haki na hawana shaka na matokeo yaliyotolewa.
Aidha, amesema umoja huo unalaani vikali kauli za baadhi ya viongozi wa siasa wanaohamasisha fujo na kusema hawajakubaliana na matokeo ya uchaguzi.
Hata hivyo, amewasihi wananchi kukaa na kushirikiana na Rais wa Awamu ya Nane kwani muda wa siasa umekwisha na sasa ni muda wa kuleta maendeleo na kuukuza uchumi kama alivyosema Rais Dkt.Hussein Mwinyibbaada ya kuapishwa jana, “Kama nilivyozungumza wakati wa kupokea matokeo ya uchaguzi leo naomba nirudie, lengo letu ni kuijenga Zanzibar, Zanzibar mpya inajengwa na sisi sote, bila kujali tofauti zetu za kiitikadi”.
Nae aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Chama cha TLP, Hussein Juma Salum amesema,uchaguzi umekwisha, "wananchi tushikamane, tujenge nchi yetu ili isonge mbele”.
Umoja huo ni muunganiko wa vyama tisa vya upinzani nichini ikiwemo UPDP, UMB, CCK, TPLB, NRA, NLD, DP, NLD na DEMOKRASIA MAKINI.
Amewataka wanasiasa kuacha kuwadanganya wananchi na kuwapotezea muda kwa madai kwamba uchaguzi utarudiwa kutokana na shinikizo na matakwa ya mataifa ya nje.
”Si kweli wananchi wanachowaambia wanasiasa kwamba uchaguzi utarudiwa kutokana na matakwa ya mataifa ya nje ambao wanadai kwamba uchaguzi haukuwa huru na haki. Zanzibar ni nchi inayoongozwa kwa mujibu wa katiba na sheria zake,”amesema.
Tags
Zanzibar