Wabunge wateule wapangua madai ya kwenda kupiga makofi bungeni

Mbunge Mteule wa Jimbo la Makete kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Festo Richard Sanga amesema wabunge wateule wanaotokana na CCM hawatakwenda kupiga makofi na badala yake watakosoa kistaarabu,anaripoti Mwandishi Diramakini.

Sanga ameyasema hayo leo Novemba 9,2020 alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari katika viwanja vya Bunge mara baada ya kujisajili bungeni humo akijibu tuhuma zinazotolewa na baadhi ya wapinzani kwamba Bunge la 12 halitakosoa kwa sababu wabunge wengi wanatokana na chama tawala.

Festo Richard Sanga.

“Hatutakwenda kupiga makofi, kauli mbiu ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli inasema ‘Hapa Kazi Tu’, hii ni Serikali ya kazi, waziri asiyefanya kazi hatutampigia makofi, tutapaza sauti kuliko wale waliokua wakipinga miradi ya maendeleo,”amesema Sanga.

Naye mbunge mteule wa Viti Maalum CCM Mkoa wa Kagera, Neema Lugangira amewataka wapinzani waheshimu maamuzi ya wananchi.

“Tuheshimu maamuzi ya wananchi, dhana ya kusema Bunge hili halitakosoa ni dhana inayolenga kutudhoofisha, nitakosoa, ni jukumu langu kuwasemea wanawake na mashirika yasiyo ya Serikali kwa sababu ndio walionituma,"amesema Lugangira.

Kwa upande wake, Mbunge Mteule wa Malinyi kupitia CCM,Antipas Mgungusi amesema Bunge la 12 halitakuwa na matusi kama ilivyozoeleka na kwamba hawatasusia mijadala yenye maslahi kwa Taifa.

“Hatuwezi kunyamaza kama watu wanavyodhani, tutakosoa, tutashauri na kupongeza pale itakapohitajika, hakutakuwa na matusi kama tulivyozoea,”amesema Mgungusi .

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news