Waislamu wajitolea kulinda makanisa Ufaransa

Kundi moja la vijana wa dini ya Kiislamu nchini Ufaransa limejitolea kulinda usalama wa makanisa nchini humo huku wakisisitiza kuwa umoja na mshikamano ndiyo dhamira yao baina ya Waislamu na Wakristo,anaripoti Mwandishi Diramakini.
Hatua hiyo ya mshikamano na umoja inakuja, licha ya hatua na matamshi ya chuki yaliyotolewa na viongozi wa Ufaransa dhidi ya Uislamu hivi karibuni.

Kwa mujibu ABC News, kundi hilo kutoka jamii ya Waislamu wa Ufaransa hususani vijana wamejitolea kulinda makanisa na hujuma na mashambulio ya kigaidi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baada ya shambulio la kigaidi lililotokea Oktoba 29, mwaka huu ndani ya Kanisa la Notre Dame katika mji wa Nice Mashariki mwa Ufaransa na kusababisha vifo vya watu wasiopungua watatu.

Aidha, katika hatua ya kuonyesha mshikamano na Wakristo wa nchi hiyo,Waislamu wamekuwa wakijumuika pamoja katika siku za mwisho wa wiki kulinda kanisa kuu la mji wa Lodève Kusini mwa nchi hiyo.

Hatua hiyo ya vijana hao wa Kiislamu imewapa moyo viongozi wa kanisa hilo ambao wameielezea kuwa ni hatua yenye kutia matumaini makubwa na mshikamano baina ya Waislamu na Wakristo.

ABC News imeongeza kuwa, kwa mtazamo wa jamii ya Waislamu wa Ufaransa shambulio la karibuni liliofanywa na mtu mmoja kwa kutumia silaha baridi ndani ya kanisa la Notre Dame huko mjini Nice halina uhusiano wowote na Uislamu.

Hata hivyo, itakumbukwa kuwa baada ya kuuawa mwalimu mmoja wa Kifaransa aliyeonyesha darasani picha za vikatuni vya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW, Rais wa Ufanransa Emmanuel Macron aliunga mkono kuendelea kuchapishwa vikatuni hivyo kwa kisingizio cha uhuru wa kutoa maoni.

Madai hayo ya Rais Macron yalichochea mashambulio kadhaa ya kigaidi ndani ya Ufaransa.Lakini mbali na nchini humo, msimamo huo wa kiongozi huyo umelaaniwa vikali na Waislamu katika kila kona ya Dunia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news