Meneja wa Wakala wa Majengo Mkoa wa Ruvuma (TBA), Mhandisi Elias Tilya ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuelezea kazi ambazo zimefanyika kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Amesema kuwa, katika jukumu la kusimamia kazi za ujenzi au ukarabati wa majengo ya Serikali na taasisi zake wamekuwa wakikutana na changamoto ya wakandarasi ambao sio waaminifu hali ambayo imekuwa ikichelewesha ukamilishaji wa miradi.
“Utakuta Mkandarasi unamlipa fedha kwa ajili ya kukamilisha kazi ya ujenzi wa mradi X yeye anachukua fedha ile na kuipeleka kwenye mradi wake mwingine, jambo hilo limekuwa likichelewesha kukamilisha kwa mradi husika pia wakati mwingine hupelekea ama kusitisha mkataba na kumpa mkandarasi mwingine au kutoa onyo kwa mkandarasi husika,"amesema Mhandisi Tilya.
Pia Mhandisi Tilya amesema kuwa, kwa sasa jengo la ghorofa la nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyasa limekamilika na linatumika, pia jengo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba limekamilika na kwa sasa linatumika.
Ameeleza kuwa, ujenzi wa jengo la utawala la Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa ambalo Mkandarasi ni SUMA JKT ambapo TBA ni wasimamiza wa mradi huo unaendelea vizuri na hatua za ujenzi.
Mhandisi huyo amesema kuwa, mradi mwingine ambao TBA wanausimamia ni ukarabati wa maabara ya maji katika Bonde la Mto Nyasa ambapo kwa muda mrefu ukarabati huo ulisimama kutokana na sababu za kiufundi katika mkataba ila kwa sasa unaendelea mbapo mkandarasi ni Kampuni ya Intercity ya jijini Dar es Salaam.
Meneja huyo amefafanua kuwa, ipo miradi ya mbalimbali ambayo TBA wanaisimamia au wanaijenga na wanakabiliwa na changamoto ya usafiri, kwani gari walilonalo ni chakavu na muda mwingi linahitaji marekebisho jambo ambalo linapelekea kutokuwa na ufanisi stahiki katika kutekeleza majukumun yao.
Amesema, changamoto nyingine ambayo wanakabiliana nayo ni maduka mengi kutokuwa na vifaa vya ujenzi ambavyo vinatakiwa kwenye mkataba husika, hali ambayo inawalazimu kuviagiza kutoka nje ya Ruvuma na kusababisha miradi hiyo ujenzi wake kuzorota au kuchelewa.