Data nchini Marekani zinaonyesha kuwa rekodi ya upigaji kura mapema
nchini humo imevunjwa baada ya watu milioni 90 kushiriki zoezi hilo la
kumchagua rais kufikia sasa, anaripoti Mwandishi Dirmakini.
Haya yamefanyika wakati Rais Donald Trump na mpinzani wake wa chama cha Democratic, Joe Biden wakiwa wanafanya kampeni kote nchini humo kujaribu kuwavutia upande wao wapiga kura waliosalia ambao hawajaamua ni nani watakayempa kura yao.
Idadi kubwa ya waliopiga kura mapema ikiwa ni asilimia 65 ya wapiga kura wote walioshiriki zoezi hilo mwaka 2016 inaonyesha jinsi kinyang'anyiro hicho kilivyo kikali huku zikiwa zimesalia siku mbili tu za kampeni.
Aidha, hofu ya kuambukizwa virusi vya corona (COVID-19) katika milolongo mirefu ya upigaji kura siku ya Jumanne ni mojawapo ya sababu zilizochangia pia kwa watu wengi kushiriki upigaji kura wa mapema.Kura za maoni zinamuonyesha Donald Trump akiwa nyuma ya Joe Biden kitaifa, lakini ushindani ni mkali katika majimbo muhimu ambayo ndiyo yatakayoamua mshindi wa uchaguzi huo nchini Marekani Novemba 3,mwaka huu.