NECTA yaweka wazi ratiba ya mitihani ya Kitaifa 2020

Leo Novemba 8, 2020 Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limesema kuwa jumla ya wanafunzi 646,148 wamesajiliwa kufanya mitihani ya Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili (FTNA) kuanzia kesho Novemba 9 hadi Novemba 20, mwaka huu, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt.Charles Msonde amesema jumla ya wanafunzi hao 646,148 kati yao wavulana ni 301,831 sawa na asilimia 46.71 na wasichana 344,317 sawa na asilimia 53.29 ambao wanatarajiwa kufanya mitihani hiyo nchini.

Pia amesema,wapo wanafunzi wenye mahitaji maaalum 731 na kati yao 406 ni wenye uoni hafifu,55 wasioona, watatu wenye ulemavu wa kusikia na 267 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili. Katibu huyo amesema, mwaka 2019 idadi ya waliosajiliwa walikuwa 609,502 hivyo kuna ongezeko la jumla ya watahiniwa 36,646 sawa na asilimia 5.7 kwa mwaka 2020 ukilinganisha na mwaka jana.

Amesema, Novemba ya kila mwaka huwa ni mwezi wa upimaji na mitihani mbalimbali ya kitaifa,upimaji wa Kitaifa wa Darasa la  Nne (SFNA) ambao utafanyika Novemba 25 na26, mwaka huu upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili (FTNA) kuanzia Novemba 9 hadi 20, mwaka huu.

Sambamaba na mtihani wa Kidato cha Nne na Maarifa ambao utafanyika Novemba 23 hadi 11 Desemba, 2020.Katibu Mtendaji huyo amesema, dhana ya upimaji wa kitaifa hutofautiana na ile ya Mitihani ya Taifa kwa kuwa upimaji wa kitaifa hufanywa katikati ya mafunzo wakati mitihani ya kitaifa hufanyika mwishoni mwa mafunzo.

Pia amesema, maandalizi kwa ajili ya upimaji na mitihani hiyo yamekamilika na kusambazwa kwa mitihani, vijitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu upimaji na mitihani katika mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani. 

Amesema, kwa upande wa Kidato cha Nne watahiniwa 490,103 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu ambapo kati yao watahiniwa wa shule ni 448,164 na watahiniwa wa kujitegemea ni 41,939,ambapo mtihani huo utaanza kufanyika Novemba 23 hadi Desemba 11, 2020.

Dkt. Msonde amesema,kati ya hao watahiniwa wa shule 448,164 waliosajiliwa wavulana ni 213,553 sawa na asilimia 47.7 na wasichana 234,611 sawa na asilimia 52.3, watahiniwa wenye mahitaji maalum 893 na kati yao 425 ni wenye uoni hafifu,60 wasioona,186 wenye ulemavu wa kusikia,na 222 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili. Pia ameongeza kuwa,watahiniwa wa QT ni 9,426 ambao wamesajiliwa kufanya mtihani wa maarifa ambapo wanaume  ni 4,147na wanawake ni 5,279 na mwaka 2019 idadi ya watahiniwa wa mtihani na maarifa waliosajiliwa walikuwa 12,984 hapa nchini.

Akizungumzia kwa upande wa Darasa la Nne amesema, jumla ya wanafunzi 1,825,679 wamesajiliwa kufanya upimaji wa kitaifa wa darasa la nne kati yao wavulana ni 909,068 na wasichana ni 916,611,katika upimaji huo watahiniwa wenye mahitaji maalum ni 4,329 ambapo kati yao 780 ni wenye uoni hafifu,103 ni wasioona,1,025 wenye ulemavu wa kusikia na 2,421 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili.

Amesema kuwa, mwaka 2019 idadi ya watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 1,783,638 hivyo kuna ongezeko la jumla ya watahiniwa 42,041 sawa  na asilimia 2.30 kwa mwaka 2020 ikilinganishwa na mwaka jana.

Dkt. Msonde amesema, mtihani huo utaanza kufanyika kuanzia Novemba 25 hadi 26, mwaka huu na  upimaji wa kitaifa wa darasa la nne huwezesha kujua kiwango cha wanafunzi wanaomudu stadi za juu za kusoma,kuandika na kuhesabu nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news