Wanafunzi wapatao 99 ambao walisoma na kuhitimu kwa miaka tofauti katika Shule ya Sekondari Kahunda iliyoko Buchosa Wilaya ya Sengerema wamejenga jiko la shule hiyo pamoja na choo chenye matundu manne vyenye thamani ya shilingi milioni 17, anaripoti Robert Kalokola (Diramakini), Geita.
Wanafunzi wa zamani waliosomea shule ya sekondari Kahunda wakiwa kwenye picha ya pamoja mbele ya Jengo la jiko wanalo jenga kwa kuchangishana ili kusaidia miundombinu ya shule hiyo. (DIRAMAKINI).
Shule ya Sekondari Kahunda ni shule kongwe iliyoanzishwa mwaka 1948 na inamilkiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).Kutokana na ukongwe wake,shule hiyo inakabiliwa na ubovu na uchakavu wa miundombinu.
Baadhi ya wanafunzi ambao walisomea shuleni hapo wamejenga jiko la shule hiyo kwa gharama ya shilingi milioni 12 .6 na choo cha wavulana kwa shilingi milioni 4.9.
Kiongozi wa wanafunzi hao ambao kwa sasa kila mmoja anafanya kazi tofauti tofauti ndani ya Tanzania, Emmanuel Magese amesema kuwa, waliamua kujenga jiko na choo kwa kuzingatia umuhimu wake shuleni hapo.
Amesema, kabla hawajafikia uamuzi huo,walishirikisha uongozi wa shule na kufikia makubaliano ya kujenga choo na jiko.
Jiko la zamani Shule ya Sekondari Kahunda. (DIRAMAKINI).
Magese amesema kuwa, jiko la shule hiyo limechakaa sana na halina viwango vya kuendelea kutumika na vyoo vya shule hiyo ni vibovu hivyo wao kama wadau muhimu waliowahi kupata elimu shuleni hapo wakaona warudishe mchango kidogo ili kuimarisha miundombinu hiyo.
Pamoja na kujenga jiko hilo na choo cha matundu manne,pia wametoa vitabu vya masomo mbalimbali ambavyo wamesema vitasaidia kupunguza upungufu wa vitabu katika shule hiyo.
Mkuu wa shule hiyo, Jose Kayuni ameseme kuwa shule hiyo ilikuwa na tatizo kubwa la ukosefu wa choo cha wavulana kwa sababu kilichokuwepo kilibomoka na kusababisha wanafunzi kutumia vyoo vya bwenini wakati wakiendelea na masomo darasani.
Amesema , wanafunzi hao wa zamani waliowahi kusomea shule hiyo wanajenga choo chenye matundu manne ambayo yatasaidia kuokoa afya za wanafunzi hao na kuondoa usumbufu wa kutembea umbali mrefu kutafuta vyoo vya mabwenini.
Mpishi wa shule hiyo, Tabu Benadeta Mkungu amesema kuwa, jiko ambalo anatumia kupikia chakula cha shule hiyo ni chakavu na linahatarisha afya za wanafunzi, lakini wanalazima kulitumia hivyo hivyo kwa sababu shule hiyo imekuwa ikibadilishiwa uongozi wa kusimamia shule hiyo mara kwa mara hivyo kuzorotesha huduma nzuri za miundombinu ya shule.
Jengo jipya la jiko la shule ya sekondari Kahunda Halmashauri ya Buchosa linalojengwa na wanafunzi waliowahi kusomea shuleni hapo. (DIRAMAKINI).
Amesema kuwa, msaada uliotolewa na wanafunzi hao wa zamani kwa kujenga jiko jipya kutasaidia kunusuru afya za wanafunzi wanaoendelea na masoma katika shule hiyo.
Mwanafunzi Keneth Moses kidato cha tatu ameieleza DIRAMAKINI kuwa, jiko la shule na choo cha wavulana vilijengwa muda mrefu, hivyo vimechakaa sana na vinatishia maisha yao.
Amesema, choo kimeshabomoka, hivyo kinahatarisha maisha ya wanafunzi katika shule,hivyo ameshukuru wanafunzi wa zamani waliokuja kuwajengea choo hicho.
Kwa upande wa jiko amesema kuwa, afya za wanafunzi zilikuwa hatarini kutokana na jiko hilo kuwa bovu na kuwa na mazingira yasiyoridhisha.
Shule ya Sekondari Kahunda ilijengwa tangu mwaka 1948 na Shirika la Wamisionari wa Kanisa la Africa Inland Church Mission na kwa sasa inamilkiwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM.
Choo cha wavulana shuleni ya Sekondari Kahunda inayomilikiwa na jumuiya ya wazazi CCM iliyoko Halmashauri ya Buchosa Wilaya ya Sengerema kilicho bomoka kutokana na kujengwa muda mrefu. (DIRAMAKINI).
Kutokana na shule hiyo kujengwa muda mrefu na kuendeshwa na watu tofautitofauti imesababisha miundombinu ya shule hiyo kuchakaa hivyo kuhitaji kufanyiwa ukarabati ili kuendana na mahitaji ya elimu kwa sasa.
Tags
Habari