Watanzania uchaguzi umeisha, sasa tulijenge Taifa letu

Hatimaye baada ya safari ya michakato ya takribani zaidi ya miezi miwili, ilihitimishwa wiki iliyopita baada ya Rais mteule wa wananchi, Dkt. John Pombe Magufuli kuapishwa na kuanza rasmi majukumu yake ya Urais kwa awamu ya pili, anaripoti Bwanku M Bwanku.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiwa na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan. 

CCM kupitia kwa Mgombea wake wa Urais ambaye sasa ndiye Rais wa Tanzania na viongozi wengine waandamizi wa chama hiko, wabunge, madiwani na wanachama wake walizunguka nchi nzima na maeneo yao kunadi sera za CCM pamoja na Ilani yake ambayo ni kubwa sana kuliko ilani zote zilizowahi kuandikwa na CCM. 

Katika historia ya CCM toka kuzaliwa kwake miaka 43 iliyopita, uchaguzi wa mwaka huu ndiyo umevunja rekodi kwa chama hicho kuandika Ilani kubwa kuliko yoyote ile. 

CCM imeweka vipaumbele vyake kwenye Ilani yenye kurasa 303 na Sura 10 zilizogusa sehemu zote za maisha ya Mtanzania na kuwa Ilani kubwa kuliko ya chama chochote kile kati ya vyama vyote 15 vilivyoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Hii ina maana gani? Hii inamaanisha kwamba CCM imeahidi mambo mengi sana kwa wananchi na sasa inapaswa kuyatekekeleza hayo ili kukata kiu ya wananchi kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa sana. Hayo ndiyo yatakuwa kipimo cha CCM baada ya miaka mitano kutokea sasa. 

Kwa ilani hii kubwa kabisa na sera zote zilizonadiwa kote nchini, ni dhahiri inahitajika nguvu kubwa sana kuitekeleza ili kukidhi haja na hamu ya Watanzania kuondolewa kero zao na kuleta maendeleo. 

Kwa misingi hiyo, wote waliochaguliwa kuanzia wabunge, madiwani na wale wote watakaoteuliwa na kupewa nafasi kwenye serikali hii wanapasa kuchapa kazi isiyo ya kitoto.

Huu sio muda tena wa kushangilia ushindi au kuzodoana ama kutambiana na mtu kwa ushindi mkubwa na wa kihistoria ambao CCM umeupata. 

Huo muda ulishapita, muda uliopo ni mara moja kuanza kushugulika na kero za wananchi na kuleta maendeleo.

Toka mfumo wa vyama vya siasa uanze mwaka 1995, uchaguzi huu wa 2020 ndio pekee ambao wananchi wametoa imani kubwa sana na ambayo haijawahi kutokea kwa CCM. 

Sio tu kwa Rais aliyepata asilimia 84.4 ya kura zote, lakini idadi kubwa ya wabunge na madiwani zaidi ya asilimia 98 kote nchini ambayo wananchi wamewapa CCM. Hii ni imani kubwa sana.

Imani hii kubwa ya wananchi inapaswa kwa nguvu kulipwa kwa kuwatumikia wananchi kwa unyenyekevu na nguvu kubwa sana. 

Rais Magufuli ana maono makubwa sana ya kuwaletea maendeleo wananchi kama alivyofanya miaka mitano ya nyuma, sasa wachaguliwa wenzake wote na wateule wanapaswa kumsadia Rais huyu sasa kutimiza azima yake na hamu ya Watanzania.

Kazi sasa ianze. Miaka mitano ni michache sana, hakuna tena muda wa siasa na longolongo, Watanzania wanataka maendeleo. 

Tumepoteza siku nyingi sana kwenye majukwaa ya siasa, twende sasa tukafukie mashimo kwa kuchapa kazi na kutekeleza yote tuliyowaahidi Watanzania. Uchaguzi umeisha! Uchaguzi umeisha! Uchaguzi umeisha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news