Watanzania wameungana na mamiloni ya watu Duniani kote kufuatilia kwa karibu mchakato wa Uchaguzi na matokeo ya uchaguzi mkuu nchini Marekani wenye ushindani mkali.
Kuna uwezekano wa kesi nyingi zaidi kufikishwa mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo, hali ambayo inaweza kuchelewesha matokeo rasmi kwa wiki kadhaa.
Baadhi ya wachambuzi wa siasa nchini Marekani, na makundi ya kutetea haki za kiraia yameonya kwamba hatua ya Rais Donald Trump kujaribu kujitangaza mshindi wa uchaguzi huo kabla ya mchakato kumalizika ni kinyume cha kanuni za kidemokrasia za Marekani.
Viongozi kadhaa duniani wapo kimya kuangalia danadana za kisiasa nchini Marekani.
Mwaka 2000, matokeo ya uchaguzi mkuu yalichelewa kutolewa baada ya kesi kufikishwa mahakamani kujua mshindi wa jimbo la Florida kati ya Rais George Bush na mpinzani wake Al Gore. Hatimaye Bush alitangazwa mshindi wa urais nchini humo.