Habari zilizotufikia kutoka vyanzo vya karibu ni kwamba aliyekuwa Mbunge wa Moshi Vijijini mwaka 2005 hadi 2015, Waziri wa Viwanda na Biashara, Msaidizi wa Rais Masuala ya Uchumi (Hayati Rais Benjamin Mkapa ) akitokea REPOA na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St. John Dodoma, Dkt. Cyril Chami, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo jijini Dodoma, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mchumi Dkt.Chami atakumbukwa kwa mengi, ikiwemo michango mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi wa Jimbo la Moshi Vijijini na Watanzania kwa ujumla.
Dkt. Cyril Chami amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Alhamisi Novemba 5, 2020 katika Hospitali ya Benjamini Mkapa jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu.
Alilazwa kwa siku kadhaa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na jana alihamishiwa hospitali ya Mkapa ambapo mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Ernest Ibenzi amesema walimhamisha Dkt. Chami baada ya kugundua kuwa figo zake zimeanza kupoteza nguvu na wakashauri aende kupata matibabu zaidi.
Dkt. Chami mwaka 2006 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kwa siku za hivi karibuni alikuwa akifundisha Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Idara ya Uchumi.
Februari 2008 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko na alikuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko mwaka 2010 hadi 2012.
Tags
Habari