Wazazi Serengeti watakiwa kutoutumia mwezi Desemba kukeketa mabinti

NA FRESHA KINASA

Katika kuelekea mwezi Desemba,2020 ambapo shule za msingi na sekondari nchini hufungwa na wanafunzi kuwa likizo, wazazi na walezi wilayani Serengeti mkoani Mara wamehimizwa kutotumia mwanya huo kuwakeketa mabinti wa kike ikiwa ni maandalizi ya kuwaozesha, badala yake wawalinde dhidi ya ukatili huo waweze kusoma na kutimiza ndoto zao kama ambavyo Serikali imekuwa ikisisitiza wakati wote.
Askari kutoka Dawati la Jinsia Wilaya ya Serengeti mkoani Mara,Sijali Nyambuche akiwapa zawadi wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ngoreme iliyopo wilayani humo baada ya kutumbuiza wakati wa kampeni ya kuelimisha wanafunzi juu ya madhara ya ukeketaji inayoendeshwa na Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania kwa kushirikiana na dawati hilo, Ustawi wa Jamii na Ofisi ya Maendeleo ya Jamii ilipobisha hodi shuleni hapo. (DIRAMAKINI).

Mwezi Desemba hutumiwa na baadhi ya wazazi na walezi kutoka koo mbalimbali za kabila la Kikurya ikiwemo Wailegi, Wakenye, Walinchoka na Wanyabasi kuwafanyia ukeketaji mabinti wao, licha ya Serikali na wadau mbalimbali kuendelea kupinga ukeketaji kutokana na madhara ya kitendo hicho kwa mabinti kwani huchangia ndoa za utotoni, kukatisha masomo yao, kutokwa damu nyingi wakati wa kukeketwa na kupelekea kifo pamoja na hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza mfano UKIMWI iwapo ngariba atatumia kifaa kimoja kukeketa mabinti zaidi ya mmoja.

Wito huo umetolewa Novemba 5, mwaka huu 2020 na Emmanuely Goodluck ambaye ni Mratibu wa Elimu ya Ukatili kutoka Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania linalojishughulisha na kutoa hifadhi kwa watoto wa kike wanaokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni lililopo Mugumu wilayani humo wakati akitoa elimu katika shule mbalimbali za msingi na sekondari.

Huo ukiwa ni mwendelezo wa kampeni ya kuelimisha wanafunzi madhara ya Ukatili hususan ukeketaji inayoendeshwa na shirika hilo kwa kushirikiana na Dawati la Jinsia, Ustawi wa Jamii na Ofisi ya Maendeleo ya Jamii wilayani Serengeti na jumla ya shule 60 zitafikiwa.
Mwelimishaji kutoka Ofisi ya Ustawi wa Jamii Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Judith Alphonce akitoa elimu ya madhara ya ukatili wa Kkjinsia ikiwemo ukeketaji kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mesaga. Kampeni hiyo inaendeshwa na Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania kwa kushirikiana na Dawati la Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii na itazifikia shule 60 wilayani humo. (DIRAMAKINI).

"Mwezi Desemba koo nyingi zinatarajia kutumia likizo kukeketa, kitendo hicho ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za nchi, ukeketaji una madhara mengi kwa hiyo niwaombe wazazi na walezi wanaotamani kuwakeketa mabinti zao waache, badala yake waone mila hiyo imepitwa na wakati na pia huchangia watoto kukatiza masomo kwani binti anapokeketwa huandaliwa kuozeshwa, nisisitize kila mwananchi awe balozi wa kuwalinda watoto wa kike na kutoa taarifa haraka pindi anapoona kuna dalili za binti kukeketwa kusudi sheria ichukue mkondo wake haraka kabla kitendo hakijatendeka,"amesema Goodluck.

Pia, Goodluck amwataka wanafunzi wanaopewa elimu hiyo kuwaelimisha wengine madhara ya ukatili hususan ukeketaji ambao utafanywa kipindi cha mwezi Desemba, huku akibainisha kuwa shirika hilo kwa kushirikiana na Serikali limejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba linakabiliana na watakaojihusisha na ukatili huo na kwamba wanakamatwa kabla ya azma yao kutekelezeka na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Naye Judith Alphonce kutoka Ofisi ya Ustawi wa Jamii Wilaya ya Serengeti akitoa elimu ya madhara ya ukatili katika Shule ya Msingi Mesaga iliyopo wilayani humo amewaomba wanafunzi wa shule hiyo kuwa tayari kutoa taarifa kwa walimu wao, ofisi ya Serikali ya kijiji, polisi ama Dawati la Jinsia kwa haraka pale mzazi ama mlezi anapokuwa katika maandalizi ya kuwasiliana na Ngariba kwa ajili ya kufanya ukeketaji ili kuweza kuokolewa kabla kitendo hakijafanyika.

Neema Getera ni mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Ngoreme iliyopo wilayani Serengeti amepongeza hatua ya Shirika la Hope kwa kushirikiana na Serikali kupeleka kampeni ya kutoa elimu ya madhara ya ukatili katika shule mbalimbali, aliomba elimu hiyo ifikishwe kwenye makundi yote ndani ya wilaya hiyo ikiwemo wazee wa kimila ambao alidai wakielimishwa vyema wana uwezo wa kusitisha ukeketaji kutokana na wao kuaminika zaidi katika kuendeleza mila hiyo.

Naye Mwalimu Girihonda Masanja wa Shule ya Sekondari Ngoreme, ameomba elimu hiyo iwe endelevu na ifanyike mara kwa mara katika maeneo yote hususan vijijini ambako ukeketaji hufanywa kwa siri, akaomba pia mabango yenye jumbe za kutoa elimu ya madhara ya ukeketaji yaweze kubandikwa sehemu mbalimbali zenye mikusanyiko ya watu kwani yaliyopo kwa sasa mengi yamechanika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news