World Vegetabe Center ya Arusha yafanikiwa kutunza aina 3000 za mbegu

Serikali imetoa pongezi kwa taasisi ya World Vegetable Center ya Arusha kwa kufanikiwa kuwa na benki ya mbegu na kutunza aina 3000 ya mbegu za mboga mboga zinazoweza kutumika kwa miaka 20 ijayo zikiwa na ubora, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Pongezi hizo za serikali zimetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya Novemba 7, 2020 alipofanya ziara ya kikazi mkoani Arusha ambapo amekagua utendaji kazi wa taasisi hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (wa kwanza kulia) akitazama shamba la majaribio ya utafiti wa mbogamboga alipotembelea kituo cha World Vegetable Center jijini Arusha.

Kusaya amesema kuwa, Taasisi ya World Vegetable Center ina makubaliano na Wizara ya Kilimo yaliyoingiwa mwezi Julai, mwaka huu yanayohusisha ukusanyaji, uchakati na utunzaji wa mbegu za mboga mboga hususan zenye asili ya Tanzania na Afrika.

“Nimeridhishwa na utendaji kazi za watafiti wa mbegu za mboga mboga unaofanywa na kituo cha World Vegetable Center na wito wa serikali ni kuwa kituo hiki kiweze kukusanya mbegu bora nyingi na kuzitunza kwa zaidi ya miaka 100 ijayo,“ amesisitiza Kusaya.

Katibu Mkuu huyo wa Kilimo ameongeza kusema kuwa, kituo hicho kupitia mkababa wa mashirikiano na Wizara umewezesha taifa kuwa na uhakika wa mbegu za mboga mboga na matunda kwa kutumia utaalam wa kisayansi ikiwemo benki ya mbegu ( genebank).

Kusaya amekitaka kituo hicho kuongeza wigo wa kufundisha vijana wengi toka vyuo vya mafunzo ya kilimo (MATIs), na vyuo vikuu ili waapte weledi wa kisayansi katika mbinu mpya za utafiti wa mbegu na udhibiti wa magonjwa na visumbufu vya mazao kupitia maabara yake ya kisasa.

Aidha, Katibu Mkuu Kusaya amesema, utekelezaji wa kazi za kituo cha World Vegetable Center ujikite katika Mpango wa Program ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP II) ili sekta ya kilimo mazao ikue na kutoa mchango mkubwa wa kiuchumi.

“Serikali kupitia wizara ya Kilimo inalenga kuwa na Afisa Ugani kila kijiji ili wakulima waweze kupata elimu bora na kanuni za kuongeza tija na uzalishaji bora wa mazao unakidhi mahitaji ya soko,” amesema Kusaya.

Ili kufanikisha mpango huo, Wizara ya Kilimo imeanzisha mfumo unaoitwa Mobile Watafiti unaolenga kuwafundisha maafisa ugani vijijini mbinu bora za kukabiliana na changamoto za uzalishaji wa mazao ikiwemo mbegu bora, udhibiti wa visumbufu vya mazao,pembejeo na huduma za ugani.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya World Vegetable Center Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Gabriel Rugalema amesema, taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 1992 na imefanikiwa kutafiti na kutunza mbegu zaidi ya 3,000 za mboga mboga zenye asili ya Afrika.

Dkt. Rugalema ameongeza kuwa, Tanzania inazalisha asilimia tano tu ya mbegu za mazao ya mboga mboga zinazotakiwa kila mwaka, hivyo kituo kimelenga kukuza uwezo wa nchi kutafiti na kuzalisha mbegu za mboga kwa ushirikiano na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI).

“Tumefanikiwa pia kuwafundisha wakulima na maafisa ugani wapatao 25,142 nchini Tanzania kupitia kituo chetu cha World Vegetable Center hapa Arusha,"amesema Dkt. Rugalema.

Kituo kimefanikiwa kuzalisha na kuachia aina za mbegu kama nyanya (6), mchicha (5), kabeji isiyofunga majani (sukuma wiki 2), mnafu (4), na ngogwe (1).

“Taasisi yetu imejikita katika kuwasaidia wakulima wa Tanzania bara na Zanzibar kujifunza, kuanzisha na kuendeleza ulimaji wa mboga wa kibiashara.Tayari kwa upande wa Zanzibar tumefikia wakulima 7,500,”amesema Dkt.Rugalema.

Kituo cha World Vegetable Center Kanda ya Arusha pamoja na kutoa mafunzo ya kilimo inatoa pia elimu na maonesho ya aina mbalimbali ili wakulima wajionee matumizi na faida za ubunifu na teknolojia bora za umwagiliaji wa matone (drip irrigation).

Dkt.Rugalema ametaja changamoto ya ufinyu wa ardhi ya kufanyia utafiti kwenye eneo hilo na kuomba Wizara ya Kilimo isaidie kituo kupata eneo jingine kwani eneo hilo limetumika kwa miaka 25 bila kupumzika.

Akijibu hoja hiyo,Katibu Mkuu Kusaya amemtaka Mkurugenzi wa kituo hicho kuwasiliana kwa karibu na wizara ili atafutiwe eneo kwenye mojawapo ya vyuo vya mafunzo ya kilimo (MATIs) na au kwenye vituo vya TARI kokote nchini.

Kuhusu suala la ucheleweshaji wa vifaa vya utafiti kutokana na urasimu kwenye upatikanaji wa vibali toka mamlaka za udhibiti ikiwemo Maabara Kuu, TMDA,TOSCI,TPRI na TRA, Katibu Mkuu huyo wa Kilimo ameahidi kuitafutia suluhu changamoto hiyo ili kazi za utafiti wa mbegu isikwame.

Taasisi ya World Vegetable Center awali ilifahamika kama Asian Vegetable Research and Development Center ( AVRDC) imelenga kutafiti na kuendeleza mazao ya viungo (spices) na matunda kwani katika Ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara hakuna utafiti katika mazao ya viungo na matunda hali inayopelekea wakulima kukosa masoko ya uhakika na kushindwa kuongeza uchumi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw.Gerald Kusaya (kulia) akitazama mbegu za mboga mboga zinazotunzwa kwenye benki ya mbegu ya kituo cha World Vegetable Center jijini Arusha. Kituo hicho kimehifadhi aina 3000 za mbegu za mboga mboga na matunda kwa miaka 28 tangu kilipoanzishwa. Kushoto ni Mtafiti Msaidizi wa Mbegu, Jeremia Sigalla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news