Klabu ya Yanga imekwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kutoka suluhu na Gwambina FC, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Katika mchezo huo ambao ulionekana kila upande kujiamini zaidi, dakika tisini zilikamilika kwa Yanga SC kuacha alama mbili huku ikichukua moja ambayo imewawezesha kufikisha alama 23, ikiwashusha Azam FC wenye alama 22 ambao walikuwa kileleni kwa muda.
Aidha, Yanga ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa.
Gwambina FC walikuwa wenyeji wa Yanga SC katika uwanja wao wa Gwambina uliopo Misungwi mkoani Mwanza.
Mbali na hayo huko mkoani Mara katika uwanja wa Karume, Biashara United FC walikuwa wakiminyana na timu ya Manispaa ya Kinondoni, KMC FC na mchezo huo umemalizika kwa sare ya goli 1-1.
Wenyeji Biashara United walikuwa wa kwanza kupata goli 5' kupitia kwa Lenny Kisu, aliyefungwa kwa mkwaju wa penati na KMC walisawazisha goli hilo 55' kupitia kwa Lusajo Mwaikenda.
Biashara wanafikisha alama 17 na wanapanda kwa nafasi moja kutoka nafasi ya nne mpaka ya tatu huku KMC FC wanapanda mpaka nafasi ya tano kutoka ya sita wakiwa na alama 15 kwa sasa.