Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel imezindua rasmi mfumo wa mawasiliano wa 4G kwenye Mji wa kitalii wa Bagamoyo ikiwa ni hatua ya kampuni hiyo kuboresha upatikanaji wa mawasiliano ya kawaida na Data kwa wateja wake,anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Fatma Latu (wa pili kulia,) akiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mauzo cha Airtel, Yusuph Kalufya pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Bagamoyo, Amru Mpumbwa (kushoto), Meneja Mauzo wa Airtel Kanda ya Pwani, Brighton Majwala wakiwa wameshikilia bango kuashiria kuipokea huduma ya 4G kwenye mji wa kitalii wa Bagamoyo ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa kampuni hiyo kuboresha upatikanaji wa mawasiliano kidigitali nchni.
Mbali na kuzindua mfumo huo wa mawasiliano wenye kasi zaidi hapa nchini, Airtel pia imezindua Duka litakalotumika kutolea huduma mbalimbali kwa wateja wa kampuni hiyo.
Akizindua mfumo huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Fatma Latu amesema, Airtel imekuwa mkombozi mkubwa kwenye sekta ya mawasiliano wilayani humo na kuwataka wananchi kutumia huduma za kampuni hiyo.
“Kwetu sisi wakazi wa Bagamoyo haya ni mafanikio makubwa na nina waomba tuiunge mkono kampuni hii ambayo imekuwa na mchango mkubwa kwa jamii ya wananchi wa wilaya yetu,”amesema Bi. Fatma.
Awali akitoa maelezo ya uwekezaji wa masafa hayo ya 4G meneja Biashara wa Airtel kanda ya Pwani, Brighton Majwala amesema Airtel imeamua kutekeleza ahadi yake ya kuwapatia wateja wake mawasiliano bora.
“Airtel Tanzania iliahidi kuboresha upatikanaji wa huduma zake kote nchini lakini hii leo tunaendelea kutekeleza ahadi hiyo kwa wateja wetu wa Wilaya ya Bagamoyo na Miji mingine mikubwa hapa nchini,"amesema Majwala.
Kwa upande wake Meneja Mawasiliano wa kampuni hiyo, Jackson Mmbando amesema kuwa Bagamoyo ni miongoni mwa Miji mikubwa ambayo imeunganishwa na mtandao mpana wa Airtel 4G.
“Bagamoyo ni Mji mkongwe wa kihistoria ambao unaunganishwa na matandao wa mpana wa Airtel 4G kutokana na umuhimu wa shughuli za kitalii ambazo pia zinachangia pato la Taifa.
"Kama mnavyofahamu Serikali ya Tanzania inamiliki kampuni ya Airtel kwa asilimia 49 na kampuni ya Bharti Airtel inamiliki asilimia 51. Hivyo basi maboresho ya mtandao kidijitali tunayofanya hivi sasa sanjari na ufunguzi wa Airtel money brach ni sehemu ya makubaliano ya wabia hao ya kufikisha huduma bora, nafuu na rahisi kwa wateja wake nchi nzima,"amesema Mmbando.
Aidha, Mmbando amevitaja vijiji vilivyofikiwa na mtandao wa 4G wilayani Bagamoyo kuwa ni pamoja na Nianjema, Magomeni, Kidongo Chekundu, Happifania, Kingani, Kiromo, Block P, Beach Side, StellaMaris, Adem, Kitopeni na Ukuni.
Meneja mawasiliano huyo amewaomba wateja wa Airtel kuendelea kutumia huduma zinazotewa na Airtel ikiwa ni pamoja na ofa ya Bando ya AIRTEL DABO DATA kwa watumiaji wa Smart Phone ili kupata Dabo kwa muda wa nusu mwaka kwa vifurushi vya wiki na mwezi kwa kipindi cha miezi sita.
Tags
Uchumi