Mashindano ya Ligi Soka Daraja la Tatu Mkoa wa Iringa (Asas Super League 2020/21) yameingia mzunguko wa tano katika makundi yote matatu ya A,B na C huku timu za Kalinga FC, Young Stars FC na Kidamali FC zikiongoza makundi hayo, anaripoti Mwandishi Diramakini (Iringa).
Wakati hao wakionekana kufanya vizuri, wenzao timu za Mapanda FC kutoka kundi A, Nzihi FC na Kitowo FC ziPO katika hati hati ya kushuka daraja katika ligi hiyo.
Ligi hiyo iliyojizolea umaarufu kutokana na ubora wake huku ikichezwa kwa makundi kabla ya kuingia hatua ya nane bora hadi sasa kwenye Kundi A lenye timu 8 linaongozwa na timu ya Kalinga FC yenye pointi 12 baada ya michezo 6 huku ikifuatiwa kwa karibu na timu ya Mafinga Boys FC yenye pointi 10 kutokana na michezo 5.
Timu ya Ifunda FC na Mapanda zinaendelea kushika mkia katika kundi hilo kwa kwa Ifunda kuwa na pointi 4 kutokana na michezo 5 huku Mapanda wakiwa na pointi 1 kutokana na michezo 4 waliyocheza.
Kundi B lenye timu 8 linaongozwa na Young Stars FC ambao wamejikusanyia pointi 11 kutokana na michezo 11 wakifuatiwa na timu ya Irole yenye pointi 8 kutokana na michezo 5 huku mabingwa wa zamani wa mashindano hayo, Nzihi FC wakishika mkia kwa kuwa na pointi 2 kutokana na michezo 5 wakifuatiwa na FFU wenye pointi 5.
Mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya maziwa ya Asas kwa misimu mitatu sasa imeonyesha ubora kwa kila kundi huku Kundi C likiongozwa na timu ya Kidamali FC wenye pointi 13 kutokana na michezo 6 waliyocheza hadi sasa wakifuatiwa na Ismani Fc yenye pointi 9 kutokana na michezo 5 na kwenye kundi hilo timu ya Kitowo FC wanashikiria mkia kwa kuwa na pointi 2 wakifuatiwa na Mawelewele yenye pointi 4 zote zikicheza michezo 5.
Katika mitanange iliyochezwa awali timu za Young Stars FC iliibuka na ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya wapinzani wao wanaoshika nafasi ya pili ya Irole katika mchezo uliopigwa uwanjwa wa Kichangani kwa magoli yaliyofungwa na Halfan Suleiman aliyetia kambani magoli mawili, goli la tatu likifungwa na Said Ally huku goli la Irole Fc likifungwa Omary Omary.
Mchezo mwingine ulizikutanisha timu za Kidamali FC na Mshindo FC (wabishi wa mjini) ambapo Kidamali waliweza kutumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kuibuka na ushindi wa goli moja kwa bila huku timu ya Nduli FC wakiibuka kidedea kwa kuwafunga timu ya Mtwivila City goli 2 kwa ubuyu.