Biashara United FCl imeibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliochezwa katika Uwanja wa Karume, mjini Musoma Mkoa wa Mara, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mabao yote mawili yamefungwa kipindi cha pili baada ya muda wa mapumziko kukamilika kwa timu zote kwenda vyumba vya kubadilishia nguo zikiwa hazijafungana.Wafungaji wa mabao ni Deo Mafie dakika ya 55 na Kelvin Friday dakika ya 90.
Timu ya Biashara United FC inayofundishwa na beki wa zamani wa Yanga, Mkenya Francis Baraza inafikisha alama 26 baada ya kucheza mechi 17 na kupanda hadi nafasi ya nne ikizidiwa alama tatu na Azam FC iliyocheza mechi 16.
Kocha Mkuu wa Biashara United, Baraza amesema kuwa vijana wake walifuata maelekezo aliyowapa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo jambo lililowapa matokeo mazuri.
Wakati huo huo mechi nyingine za Ligi Kuu Desemba 22,2020 bao la dakika ya 90 la kiungo wa zamani wa Simba, Peter Mwalyanzi limeinusuru Kagera Sugar kupoteza mechi nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Polisi Tanzania Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Kagera Sugar ilitangulia kwa bao la Ally dakika ya 11, lakini Polisi Tanzania ikasawazisha kupitia kwa Daruwesh Saliboko dakika ya 24 na kupata la pili dakika ya 35 kupitia kwa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Tariq Seif Kiakala.
Katika mechi nyingine Mwadui FC imelazimishwa sare ya bila kufungana na Coastal Union ya Tanga katika Uwanja wa Mwadui Complex, Kishapu mkoani Shinyanga.
Awali bao la dakika ya mwisho kabisa la Japhet Mayunga liliinusuru Gwambina kuchapwa nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Mbeya City, waliotangulia kwa bao la penalti la Kibu Dennis dakika ya 34.
Leo Desemba 23, 2020 Kocha msaidizi wa Timu ya KMC FC, Habibu Kondo amesema kuwa hadi sasa kikosi chake kipo vizuri kuelekea mpambano wake dhidi ya JKT Tanzania mchezo utakaopigwa katika dimba la Jamuhuri jijini Dodoma saa 8.00 mchana.
Ameongeza kuwa, licha ya kwamba ametoka kupoteza michezo mitatu mfululizo, lakini hivi sasa anachokiangalia ni mchezo wa leo na kwamba kikosi hicho cha wana Kino Boys, kipo katika hali nzuri na kwamba wanauwezo mkubwa wakushinda mchezo huo licha ya kwamba watakuwa ugenini.
Kocha Habibu amesema kuwa mchezo wa leo ni mwingine na kwamba anachokiangalia ni kuweka sawa mipango na wachezaji wake katika kuhakikisha kuwa anapata matokeo mazuri ikiwa ni kuchukua alama tatu dhidi ya wapinzani wake.
“Tunakwenda kucheza na timu ngumu, tunaiheshimu JKT Tanzania, lakini niseme kwamba KMC FC ndio itakayokuwa ngumu na bora kwao hatuangalii tumepoteza michezo mingapi ila tuna angalia tunapataje matokeo tukiwa ugenini hapa Jamhuri Dodoma,” amesema kocha Habibu.
Hata hivyo Habibu amesema kuwa katika kikosi chake atawakosa wachezaji wanne kutokana na kusumbuliwa na majeraha ambao ni Hassan Kabunda, Abdul Hillary, Hassan Kapalata pamoja na Reliant Lusajo.
Tags
Michezo