Corona yamuua Waziri Mkuu wa Ufalme wa Eswatini

Waziri Mkuu wa Ufalme wa Eswatini, Ambrose Mandvulo Dlamini (52) amefariki baada ya kuambukizwa virusi vya Corona (COVID-19), anaripoti Mwandishi Diramakini (Johannesburg).

Duru za habari kutoka Kusini mwa Afrika zimeieleza Diramakini kuwa, Dlamini alibainika kuwa ameambukizwa virusi hivyo,wiki nne zilizopita, hivyo kulazimika kukimbizwa nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

Ni baada ya mwenyewe pia kukiri Novemba 16, mwaka huu kuwa amethibitika kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona.

Dlamini amekuwa Waziri Mkuu tangu Novemba 2018 ambapo kabla ya hapo alikuwa Mtendaji Mkuu wa MTN Eswatini na amewahi kuhudumu katika taasisi za kibenki kwa miongo kadhaa nchini humo.

Hata hivyo, taarifa iliyoonwa na Mwandishi Diramakini kutoka kwa Naibu Waziri Mkuu imethibitisha kifo hicho;

"Wakuu wameamuru kwamba nijulishe taifa juu ya kifo cha kusikitisha na cha mapema cha Mheshimiwa Waziri Mkuu Ambrose Mandvulo Dlamini," Naibu Waziri Mkuu Themba Masuku amesema."Waziri Mkuu amefariki akiwa chini ya uangalizi wa matibabu katika hospitali moja huko Afrika Kusini,"ameongeza.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Wizara ya Afya katika ufalme wa Eswatini hadi sasa wamerekodi kesi zaidi 7,000 za maambukizi ya virusi vya Corona (COVID-19) na vifo 127.

Juhudi za Diramakini kumpata Msemaji wa Serikali, Sabelo Dlamini ili kupata muongozo zaidi bado zinaendelea kwa sasa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news