Wasanii wa Tanzania, Diamond, Nandy na Rayvany wametwaa tuzo za Kimataifa kupitia hafla iliyotangazwa na waandaaji wa African Entertaiment Awards USA (AEAUSA) zilizotolewa nchini Marekani, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Tuzo hizo huwa zinatolewa kila mwaka na zilianza kutolewa mwaka 2015 zikilenga kuheshimu ubora wa kazi za wasanii na wadau mbalimbali.
Miongoni mwa vipaumbele ni pamoja na upande wa burudani, uongozi kwa maana ya kijamii ikiwemo masuala ya ujasiriamali barani Afrika.
Katika tuzo za mwaka huu wa 2020, mwanadada Nandy ametwaa tuzo ya msanii bora wa kike barani Afrika,huku Diamond akitwaa tuzo ya msanii bora wa kiume barani Afrika kwa mwaka 2020.
Kwa upande wake, Rayvanny ametwaa tuzo ya mwanamuziki bora wa kiume Mashariki, Kusini na Kaskazini mwa Afrika kwa mwaka 2020.
Uongozi wa Diramakini Business Limited ambao ni wamiliki wa www.diramakini.co.tz unachukua nafasi hii kuwapongeza sana, vijana hawa wa Kitanzania huu ukiwa ni mfululizo wa tuzo za Kimataifa, kwani tunaamini licha ya tuzo hizi kulitangaza Taifa letu pia zinatoa hamasa kwa vijana wenye vipaji kujituma zaidi.