Dkt.Kalemani:Umeme wa uhakika ni kipaumbele chetu

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani akiwa katika kikao kazi na Bodi za Wakurugenzi za taasisi tano zilizo chini ya Wizara ya Nishati ametaja kipaumbele cha Sekta ya Nishati kwa sasa ni kuwa na umeme wa uhakika, unaotosheleza mahitaji ya nchi na ziada inayobakia kuuzwa nje ya nchi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Dkt. Kalemani amesema ili kuweza kufikia kipaumbele hicho, Bodi ya Wakurugenzi TANESCO pamoja na Menejimenti zisimamie miradi ya kuzalisha umeme inayotekelezwa ili ikamilike kwa wakati na kila mtumishi atimize wajibu wake kazini.

"Bodi mkasimamie miradi ya JNHPP, Kinyerezi I Extension ikamilike kwa wakati, lakini pia upelekaji wa umeme wa gridi ya Taifa Mikoa ya Kigoma na Katavi kutokea Tabora ikamilike ndani ya miezi nane,"amesema Dkt.Kalemani.

Ameongeza kuwa, upelekaji wa gridi ya Taifa mikoa ya Kigoma na Katavi ni lazima kwani Serikali imekuwa ikitumia pesa nyingi katika ununuaji wa mafuta ya kuendesha jenereta.

Dkt. Kalemani amesisitiza kuwa, matumizi ya umeme nchini kwa siku ni takribani megawati 1,118, huku TANESCO ikiwa na megawati 1,602.41 hali inayoonesha uhitajika wa uwepo umeme zaidi, kwani Wateja bado wanaendelea kuunganishwa.

Aidha, ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi TANESCO, Menejimenti na Wafanyakazi kwa kufanya kazi vizuri katika miaka mitano iliyopita, na kuongeza kuwa tangu mwaka 2017 TANESCO inajiendesha bila kupata ruzuku Serikalini.

Dkt. Kalemani ameitaka TANESCO kukusanya madeni kutoka kwa wadaiwa wote, tasisi za Serikali na watu binafsi, TANESCO wametakiwa kuwakatia umeme wale wote ambao hawata lipa madeni yao kwa wakati.

Dkt. Kalemani pia ameiagiza Bodi ya TANESCO kuwawekea malengo Mameneja wa Mikoa na Wilaya ili kuweza kuwapima kwa utendaji kazi wao.

Malengo hayo ni umeme kuto kukatika zaidi ya mara kwa mara, ukusanyaji wa mapato, pamoja na masuala ya utoaji huduma kwa Wateja.

Kwa upande wake Naibu Waziri Nishati, Mhe. Stephen Byabato amesema yupo tayari kumsaidia Mhe. Waziri katika kutekeleza majukumu yake.

Mhe. Byabato amewataka Watendaji wa Wizara na Taasisi zake kuwa wabunifu katika utendaji wa kazi lakini pia kuzingatia usahihi wakati wa kutekeleza majukumu ya kila siku.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi aliwapongeza Mhe. Waziri na Naibu Waziri kwa kuteuliwa kuiongoza Wizara ya Nishati.
Dkt. Kyaruzi ameeleza kuwa, maagizo yote ambayo yametolewa na Waziri pamoja na Naibu Waziri, Bodi ya TANESCO imeyachuku na itayafanyia kazi ipasavyo.

"Mhe. Waziri na Mhe. Naibu Waziri, niwakikishie Bodi ya Wakurugenzi TANESCO tutafanyia kazi yale yote ambayo mmetuagiza,"amesema Dkt. Kyaruzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news