Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amesema kuwa jeshi hilo limeanza uchunguzi dhidi ya Kampuni ya Qnet iliyotajwa maeneo mbalimbali ya nchi kwa tuhuma ya kufanya udanganyifu kwa watu mbalimbali katika biashara yake inayofanyika kwa njia ya mtandao,anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Amesema kuwa baada ya kuona malalamiko kutoka sehemu mbalimbali kuhusu kampuni amemwagiza Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, DCI Robert Boaz kufungua jalada la uchunguzi kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwa kampuni hiyo.
IGP Simon Sirro amesema hayo akiwa anazungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya nyumba za makazi ya Askari polisi eneo la mtaa wa Magogo mjini Geita alipofika kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba hizo.
Sirro amesema, jeshi hilo pia linaendelea kupambana na uhalifu wa mtandaoni (cyber crimes) ili kuukomesha na kwa sababu uhalifu huo ni mgeni hapa nchini jeshi limesomesha wataalum wa kutosha kuweza kupambana na uhalifu huo.
Katika ujenzi wa nyumba hizo za askari polisi eneo la Magogo,Sirro ameagiza kufikia Januari 2021 nyumba hizo ziwe zimekamilika na askari wawe wameanza kuishi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Geita Kamishna Msaidizi Mwandakizi Henry Mwaibambe akitoa taarifa ya ujenzi wa nyumba za makazi za Askari polisi eneo la magogo mjini Geita (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Henry Mwaibambe amesema, ujenzi wa nyumba hizo umekakamilika kwa asilimia zaidi ya 90.
Amesema, mradi huo wa makazi ya askari ulianza kwa baadhi ya wafanyabiashara wa mjini Geita kuchangia zaidi ya milioni 60 na Ofisi ya IGP kupeleka milioni 500 kujenga makazi ya askari.
IGP Simon Sirro akisalimiana na Maafisa waandamizi wa Jeshi la Polisi mkoa wa Geita pamoja na wadau mbalimbali waliochangia ujenzi wa nyumba za makazi za Askari polisi eneo la Magogo mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).
Kamanda Mwaibambe amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli kuwezesha upatikanaji wa sh.milioni 500 kwa ajili ya kujenga majengo hayo pamoja na wafanyabiashara wa Geita kuunga mkono juhudi hizo.
IGP Simon Sirro ametembelea mkoa wa Geita ambapo amekiri kuwa mkoa huo kwa sasa hauna uhalifu kama kipindi cha nyuma.
Tags
Habari