Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Mjumbe wa Baraza la Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili aweze kushiriki na kutekeleza vyema majukumu yake katika baraza hilo, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Kiapo hicho kimeshuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Viongozi kadhaa wamehudhuria hafla hiyo akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan,Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa, Mwanasheria Mkuu Adelardus Kilangi, Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi John William Kijazi pamoja na Manaibu Mawaziri na watendaji wengine wa Serikali.
Hafla hiyo imefanyika leo katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma ambapo wakati huo huo mara tu baada kiapo hicho kikao cha Baraza la Mawaziri kilifunguliwa na Mwenyekiti wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwa kula kiapo na kushiriki katika kikao hicho cha ngazi ya Juu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, Rais Dkt. Magufuli amewapongeza Mawaziri wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa ni sehemu ya Baraza hilo la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushiriki wao katika kikao hicho pamoja na kuwapongeza Manaibu Mawaziri kwa uteuzi walioupata ndani ya Serikali.
Mikutano ya Baraza hilo huongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye anayekuwa Mwenyekiti wa vikao vya Baraza la Mawaziri.
Mara baada ya kiapo hicho Rais Dk. Hussein Mwinyi alishiriki katika Kikao hicho cha kwanza katika kipindi cha pili cha uongozi wa Awamu ya Tano ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ambaye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao.
Ushiriki wa Rais Dk. Hussein Mwinyi unatokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 54 Ibara ya kwanza ambayo inawataja Wajumbe wa Baraza la Mawaziri kuwa ni Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa kifungu hicho cha 54 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la Mawaziri litakuwa ndicho chombo kikuu cha kumshauri Rais juu ya mambo yote yanayohusika na utekelezaji wa madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba.
Sambamba na hayo, kifungu hicho cha 54 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinaeleza kwamba Baraza la Mawaziri litamsaidia Rais na kumshauri juu ya jambo lolote litakalowasilishwa kwenye Baraza hilo kwa mujibu wa maagizo maalum au maagizo ya jumla yatakayotolewa na Rais.