Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesuluhisha mgogoro uliodumu kwa takriban miaka 40 ambao ulileta uhasama na chuki baina ya Shirika la Watawa wa Kikatoliki na wananchi wa kijiji cha Mlangoni katika Wilaya ya Siha mkoa wa Kilimanjaro kuhusiana na shamba la Kirari,anaripoti Munir Shemweta (WANMM) Kilimanjaro.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiwasili katika kijiji cha Kirari wilayani Siha mkoa wa Kilimanjaro kuhitimisha mgogoro uliodumu kwa miaka 40 baina ya Wananchi wa kijiji hicho na Watawa wa Shirika la Kanisa Katoliki leo tarehe 19 Desemba 2020.
Katika shamba hilo wananchi wa kijiji cha Mlangoni wanaishi eneo lenye ukubwa wa ekari 347 na Watawa kubakia na ekari 1063 ambapo kwa mara ya kwanza Hati ya shamba hilo ilitolewa tarehe 26 Oktoba, 1950 kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kilimo.
Lukuvi alifikia suluhu na pande hizo mbili baada ya kukutana na viongozi wa kijiji cha Mlangoni na Watawa wa Kanisa Katoliki kwa lengo la kutafuta suluhu baada ya Mahakama ya Rufaa Tanzania kuwapatia ushindi Watawa na hivyo kulazimu wananchi wa kijiji hicho wanaofikia 3,700 kutakiwa kuondoka katika shamba la Kirari.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alifika katika kitongoji cha Kirari leo tarehe 19 Desemba 2020 akiwa katika ziara yake ya kutembelea wilaya za Hai na Same mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya kushughulikia migogoro ya ardhi katika wilaya hizo.
Katika mkutano wake na wananchi na Watawa wa Katoliki, Lukuvi alisema katika kutafuta suluhu ya mgogoro wa eneo hilo lilokuwa limegawanywa katika hati mbili moja ikiwa na ekari 347 na nyingine ekari 1063 serikali iliamua kuingilia kati mgogoro huo ili kunusuru nyumba 268 kuondoshwa katika eneo hilo.
"Hatukuingilia wala hatupingani na hukumu ya Mahakama ya Rufani bali tumekuja ili Watawa wapate haki yao kwa njia tofauti, hii ni Win win situation,"amesema Lukuvi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akisalimiana na mmoja wa Watawa wa Kanisa Katoliki katika ofisi ya halmashauri ya wilaya ya Siha mkoa wa Kilimanjaro wakati wa mazungumzo ya kuhitimisha mgogoro wa ardhi katika Shamba la Kirari uliodumu kwa miaka 40 leo tarehe 19 Desemba 2020.
Kwa mujibu wa Lukuvi, baada ya serikali kufanya mazungumzo na Watawa kuhusiana na suluhu ya mgogoro huo, Shirika la Watawa wa Kanisa Katoliki lilikubali kuachia sehemu ya maeneo yaliyovamiwa kwa lengo la kurudishiwa thamani ya eneo husika kwa gharama za serikali.
Katika ufumbuzi wa mgogoro huo mbali na wavamizi kuamuliwa kulilipa shirika la Watawa kwa kurudishiwa thamani ya eneo husika pia Shirika hilo limekubali kulipa fidia kwa nyumba kumi zilizokuwa karibu na shirika la Watawa ili kuepuka muingiliano.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema, wananchi waliovamia shamba hilo watamilikishwa kwa hati hawatalipa tozo ya mbele (Premium) bali watalipa thamani ya ardhi pamoja na fedha ya kumilikishwa na kusisitiza kuwa eneo hilo limetengewa pia maeneo ya barabara, soko, kuzikia, shule na ofisi ya kijiji.
"Leo ni mara ya saba nakuja kushughulikia mgogoro huu wa kitongoji sasa mnaweza kufanya shughuli zenu bila wasiwasi na tunata mjenge nyuma katika viwanja vilivyopimwa,"amesema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi Watawa wamekubali kupoteza kidogo na kukubali wananchi wabaki kwa masharti ya kufidia thamani ya ardhi waliyoachiwa kwa kuwa kubomoa nyumba za wananchi ni gharama kubwa na kusisitiza fidia italipwa kwa viwango vya serikali.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Siha mkoa wa Kilimanjaro, Onesmo Buswelu amelisifu Shirika la Watawa wa Kanisa Katoliki kwa kuwa watulivu katika muda wote wa kutafuta suluhu ya mgogoro huo uliozikwa rasmi leo tarehe 19 Desemba 2020.
Wananchi wa Kirari walimshukuru Waziri Lukuvi kwa jitihada zake za kuhakikisha mgogoro huo unakwisha kwa amani na kufungua ukurasa mpya baina yao na Watawa.
Nao Watawa wa Shirika la Kanisa Katoliki walisema wao walijua hamuonei mtu wakati wa kutafuta haki na muda wote wa mgogoro waliathirika kwa kuwa walikuwa barabarani na wamekubali kusamehe gharama zote za kutafuta haki.
Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema Wizara yake sasa inakubali kusajili majina zaidi ya moja yakiwemo ya wenza katika hati za ardhi ili kuepusha matatizo ya mirathi hapo baadaye.
Lukuvi amesema hiyo ni fursa kwa wanawake kushawishi waume zao katika kutekeleza suala hilo kwa kuwa sheria iko wazi na hakuna Afisa Ardhi atakaye hoji suala hilo.
Amesema, hata mtoto chini ya miaka 18 anaweza kusajiliwa katika hati kwa masharti kuandikwa pia jina la msimamizi.
"Akina mama mna ushawishi mkubwa washawishini waume zenu waandike majina mawili ili kuepuka mgogoro hata kama una mke zaidi ya mmoja,"amesema.
Tags
Habari