Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameshusha neema kwa vijiji vitatu vya Ndungu, Msufini na Mperani vilivyopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro kwa kuvipatia ekari mia tatu kila kijiji kwa ajili ya makazi na kuagiza kufanyika ukaguzi wa mashamba makubwa nchini kubaini yasiyoendelezwa,anaripoti Munir Shemweta (WANMM) Same.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akifurahi na akinamama wa Tarafa Ndungu wilayani Same alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi baina ya Mwekezaji na wananchi wa vijiji vya Msufini, Mperani na Ndungu wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro Desemba 20, 2020.
Hatua hiyo inafuatia wananchi wa vijiji hivyo kuomba
kupatiwa sehemu ya ardhi ya Mwekezaji Kampuni ya LM Investment kwa ajili
ya makazi ambapo baada ya uamuzi sasa Mwekezaji atabakia na jumla ya
ekari 2,452.844.
Akizungumza
na wananchi wa Ndungu wilaya ya Same mkoa wa Kilimanjaro leo tarehe 20
Desemba 2020 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema,
baada ya Mwekezaji kuachiwa ekari hizo 2,452.844 anachotaka ni kuona
uwekezaji wa uhakika unafnyika na kusisitiza asipofanya uwekezaji
atanyang'anywa shamba.
Alimuonya
Mwekezaji kwa kumtaka kuhakikisha shamba lake linapandwa mkonge na
kusisitiza ardhi hiyo lazima itumike ili vijana waajiriwe na kubainisha
kuwa haiwezekani mwekezaji kuwa na ekari 2,452.844 halafu atoe ajira ya
watu 50 tu.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akikagua uzalishaji katani katika kiwanda cha mwekezaji LM INvestment Tarafa ya Ndungu wilayani Same mkoa wa Kilimanjaro alipokwenda kuvipatia vijiji vitatu ekari mia tatu za makazi Desemba 20 2020, kulia kwa Lukuvi Mkuu wa Wilaya ya Same Rosemery Senyamule.
"Hatufukuzi wawekezaji bali tunataka maendelezo katika shamba na tunataka muwekezaji kuacha kutumia mkopo kuendeleza maeneo mengine,"amesema Lukuvi.
Wananchi wa vijiji hivyo vitatu waliomba kupunguziwa ardhi kutoka kwa Mwekezaji kwa maelezo ya kutokuwa na ardhi ya kutosha kwa ajili ya makazi kutokana na ardhi yao kuwa tepetepe.\
Ombi la wananchi hao, lilisababisha Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuona umuhimu wa wananchi hao kupatiwa ardhi kwa ajili ya makazi na kupunguza sehemu ya shamba la Mwekezaji na kukipatia kila kijiji ekari mia moja.
Tayari taratibu zote za upimaji na upangaji eneo hilo zimefanyika ikiwemo kusajili ramani ya eneo hilo na wiki ijayo ofisi ya ardhi itakwenda kukabidhi ardhi kwa vijiji hivyo vitatu pamoja na mwekezaji .
Waziri Lukuvi amesema, kwa sasa ardhi ya shamba hilo imehama kutoka mikono ya kijiji na sasa wananchi wake watapatiwa hati za mjini za miaka 99 yaani hazitatolewa hati za kimila kama ilivyokuwa huko nyuma.
Amesema, Wizara yake italipanga upya eneo la shamba hilo na kusisitiza kuwa wananchi watakaomilikishwa watapaswa kuchangia gharama zote za kupanga, kupima sambamba na zile za miundombinu.
"Halmashauri na serikali ya kijiji mtakaa pamoja na kukokotoa gharama za kuchangia maana tumefanya kazi kubwa ya kuwatafutia ardhi na gharama zenyewe hazitazidi zile za mjini ambazo ni 150,000, pamoja na eneo hilo kupangwa lakini eneo ambalo wananchi wamejenga muda mrefu litarasimishwa," amesema Lukuvi.
Akigeukia suala la ukaguzi mashamba Lukuvi ameagiza kufanyika ukaguzi wa mashamba yote makubwa kwa lengo la kutaka kujua uwekezaji uliyofanyika ikiwemo kujua kiasi yanavyochangia kodi ya serikali pamoja na ajira.
Waziri Lukuvi aliagiza Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Ardhi katila mikoa kufanya ukaguzi wa haraka na kuona kama uwekezaji katika mashamba hayo una tija.
Kwa niaba ya wananchi wa vijiji hivyo, Mzee Kabongo mkazi wa Ndungu alimshukuru Waziri wa Ardhi kwa kuwezesha kupatikana kwa ekari hizo na kumupmba Lukuvi kufikiria ueezekano wa kuongeza ekari kwa vijiji hivyo.
Tags
Uchumi