Mbunge Balozi Chana kuwakatia bima wenye uhitaji maalum

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe, Balozi Dkt. Pindi Chana ameahidi kuwakatia bima ya afya kutoka Mfuko wa Afya ya Jamii iliyoboreshwa (CHF) baadhi ya watu wenye uhitaji maalum pamoja na makundi mbalimbali ili kuweza kupata matibabu kwa urahisi na kuimarisha afya zao,anaripoti Damian Kunambi (Diramakini) Njombe.
Hayo ameyasema wakati akikabidhi zawadi ya majembe yenye thamani ya sh. milioni mbili kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilayani Ludewa, Leah Mbilinyi ambapo amekabidhi majembe hayo kwa wilaya mbalimbali za mkoa huo ikiwa ni muendelezo wa utaratibu ambao amejiwekea kufanya hivyo kwa kila mwaka.
Amesema, kwa sasa ataanza na baadhi ya watu wasiojiweza waliopo katika kundi la UWT wilaya ya Ludewa na kisha ataangalia makundi mengine nje ya UWT ambao ataona wanauhitaji wa kupata msaada wa kukatiwa bima hiyo.
“Tunamshukuru sana Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuboresha huduma mbalimbali ikiwemo huduma ya afya, kwani bima hii imeboreshwa vyema na nikaona inaweza kuwa msaada mkubwa kwa watu wa makundi mbalimbali ndiomaana nikaona nitoe msaada huu ambao utawalenga watu wasiojiweza tu.

"Nitaangalia watu waliopo kwenye makundi mbalimbali ambao nitaona wana uhitaji maalum ili iweze kuwasaidia kupata huduma za afya na kumudu matibabu mbalimbali ambayo yalikuwa nje ya uwezo wao katika kuyalipia,"amesema Balozi Dkt. Pindi Chana.
Aidha, kwa upande wa mratibu wa CHF wilayani humo, Michael Kolimba amesema kuwa kwa sasa mfuko huo umeboreshwa ambapo mwanachama anaweza kwenda kutibiwa katika hospitali yoyote ndani ya Tanzania isipokuwa hospitali za rufaa tu.

Ameongeza kwa kutoa wito kwa wananchi mbalimbali kujiunga na mfuko huo kwakuwa gharama zake ni nafuu ambapo kwa shilingi elfu 30000 unapata bima ambayo itahudumia watu sita katika familia ambapo ni baba, mama na watoto wanne.
Naye Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Ludewa, Leah Mblinyi amemshukuru mbunge huyo kwa msaada huo wa bima ya afya pamoja na majembe na kusema kuwa majembe yamekuja katika kipindi sahihi kwa kuwa sasa hivi wapo katika kipindi cha kilimo.

“Tunakushukuru sana balozi Dkt. Pindi Chana kwa kutuletea zana hizi za kilimo, kwani kwa sasa tupo katika kipindi cha kilimo na huu ni msaada mkubwa kwetu kwani zitatuwezesha kuendeleza kilimo hiki na kutuletea mafanikio,"amesema Mbilinyi. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news