Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Joseph Kamonga ameliomba Baraza la Madiwani kusimamia vyema vyanzo vya mapato pamoja na kubuni vyanzo vingine ili kukuza uchumi wa wilaya hiyo, anaripoti Damian Kunambi (Diramakini) Njombe.
Hayo ameyasema katika hafla ya kuwaapisha madiwani iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya na kuongeza kuwa wasisubiri serikali itumie nguvu katika kufanikisha hilo.
Ameongeza kuwa, wanapaswa kukusanya mapato ili fedha hizo zitumike kutatua matatizo mbalimbali ikiwemo kuboresha sekta ya elimu na afya.
"Ndugu zangu tusipoweza kukusanya mapato hatutaweza kutatua changamoto za wananchi, hivyo tunapaswa kufanya hivyo kwa nguvu zote na pale patakapotokea changamoto za kisera au sheria Mimi simu yangu iko wazi muda wote msisite kunishirikisha,"amesema Kamonga.
Aidha, kwa upande wa katibu tawala wa wilaya ya Ludewa, Zaina Mlawa amewataka madiwani wote kuhakikisha kuwa mpaka kufikia Januari 30, 2020 watoto waliofaulu darasa la saba na kupangiwa shule wanaripoti katika shule walizopangiwa na kuanza masomo.
Amesema, mara nyingi idadi ya wanafunzi waliofaulu na kupangiwa shule ni tofauti na idadi ya wanafunzi wanaripoti katika shule hizo kitu ambacho kinashusha ukuaji wa sekta ya elimu katika wilaya hiyo.
"Madiwa mkisimama vyema katika nafasi zenu mnaweza kuleta maendeleo ya elimu katika kata zenu na wilaya kwa ujumla, hivyo mhakikishe mnatekeleza hili kwa ushirikiano na wazazi,"amesema Mlawa.
Kwa upande wa mmoja wa madiwani hao, Willbard Mwinuka amesema kuwa wameyapokea yote waliyoaswa na wakuu wa idara mbalimbali pamoja na mbunge na wataenda kutekeleza kwa kila hali ili kuleta maendeleo katika wilaya hiyo.
Amesema kwa upande wake amejipanga vyema katika kufanya kazi kwa bidii na atahakikisha analeta maendeleo katika kata yake na wilaya kwa ujumla.