Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Constantine Kanyasu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Constantine Morandi wamesema wamejipanga kumaliza changamoto ya uhaba wa madarasa, zahanati pamoja na maji katika Jimbo na Halmashauri ya Mji wa Geita, anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Mbunge Constantine Kanyasu amesema miaka mitano iliyopita mwaka 2015 -2020 Halmashauri ya Mji wa Geita ilijenga shule mpya 16 hivyo katika kipindi cha miaka 5 ijayo kwa 2020-2025 kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo watamaliza upungufu wa vyumba vya madarasa au kufikia asilimia 80.Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Constantine Kanyasu akiwa anachimba msingi katika ujenzi wa shule mpya katika Mtaa wa Samina Kata ya Mtakuja Geita Mjini, (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).
Kanyasu anasema hayo wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa
shule mpya ya msingi katika Mtaa wa Samina Kata ya Mtakuja Mjini Geita
ambayo yeye na mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Geita, Constantine
Morandi wameshirikiana na wananchi wa mtaa huo kuchimba msingi.
Kanyasu
anasema kuwa, shule hiyo inajengwa ili kunusuru uhai wa watoto wadogo
hasa wa madarasa ya chini kama wa darasa la kwanza kwa kutembea umbali
mrefu kufuata shule mtaa wa pili wa Mpomvu.
Amesema kuwa, wanafunzi wanatembea zaidi ya kilomita 4 kutoka mtaa wa Samina kwenda mtaa wa Mpomvu na wanapita katika barabara kuu itakayo Mwanza kuelekea Bukoba jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa wanafunzi hao.
Mbunge Constantine Kanyasu amechangia ujenzi kwa kutoa matofali 2000
kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa matatu kwa kuanzia huku
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Constantine Morandi akichangia
mifuko ya saruji 50 .
Kanyasu amesema katika kampeni za uchaguzi
mkuu mwaka huu aliahidi kujenga shule katika Mtaa huo na kwamba kwa
kuwa amepata Mwenyekiti wa Halmashauri ambaye anapenda kuona vitu
vinafanyika,watashikiana kumaliza tatizo la uhaba wa madarasa, zahanati
na kutatua changamoto ya maji.
Shule hiyo inaanza kujengwa vyumba
saba vya madarasa na ofisi mbili za walimu ambapo wananchi wameshakusanya tripu 30 za mawe na mchanga tripu 10 kwa ajili ya ujenzi huo.
Constantine Morandi ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita akishiriki kuchimba msingi wa shule mpya katika Mtaa wa Samina Kata ya Mtakuja Mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola).
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya mji wa Geita Constantine Morandi ambaye pia ni Diwani
wa kata hiyo,amesema watasimamia ujenzi huo ukamilike mapema ifikapo
mwezi Machi mwaka 2021.
Morandi amesema watoto wa mtaa huo wa
Samina walikuwa wanatembea kilomita 4 kufuata shule katika Mtaa jirani
wa Mpomvu ambapo wanalazimika kupita katika barabara kuu ya kutoka
Mwanza kwenda Bukoba ambayo ni hatari kwa usalama wa watoto hao kugongwa
na magari.
Aidha, amesema shule ya msingi ya Mpomvu ina wanafunzi
2674 kwa idadi hiyo shule inahitaji kupunguziwa wanafunzi na kati ya
hao wanafunzi 1050 wanaotoka mtaa wa Samina kwenda kufuata shule ya
Msingi Mpomvu.
Baadhi ya wananchi wa mtaa wa Samina wakishiriki katika kuchimba msingi katika ujenzi wa shule mpya inayoanza kujengwa kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Geita mjini na diwani wa kata ya Mtakuja ambaye ni mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Geita Constantine Morandi (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).
Afisa Mtendaji wa kata hiyo Neema Onesmo amesema
fedha zaidi ya milioni 100 zitatumika katika ujenzi wa shule hiyo na
kwamba kwasasa wameanza na nguvu za wananchi pamoja fedha za ruzuku
kutoka kwa vibarua wanaotoka kwenye mtaa huo na kufanya kazi GGML.
Neema
Onesmo amesema kuwa,kata hiyo ina mitaa 7 ,shule za msingi 5, hivyo
mtaa wa samina ulikuwa unategemea Mtaa wa Mpomvu na kutokana na umbali
wanafunzi wengi hasa watoto wa darasa la kwanza walikuwa wanashindwa
kufika shuleni kila siku hivyo kuwepo utoro kutokana na uchovu au
kuogopa kuadhibiwa na walimu kwa kuchelewa kila siku.
Afisa
Mtendaji wa mtaa wa Samina, Deus Bulalu wakati akisoma risala kwa mbunge
wa Jimbo la Geita mjini alisema kuwa Shule hiyo ina eneo lenye ukubwa wa
ekari 10.5 na mahitaji ya tofali za kujengea maboma 7 ni tofali 6,480
na mifuko ya saruji 162.
Ameongeza kuwa, wananchi wameisha kusanya
mawe tripu 30 ,mchanga tripu 10 na kokoto tripu 2 ambapo mtaa huo una
kaya 656 na una idadi ya watu 2804 huku wanawake wakiwa 1376 na wanaume
1428.
Zena Nalichika Mkazi wa mtaa wa Samina anasema kuwa watoto
wao wanateseka kwa kutembea umbali mrefu kwenda Mpovu lakini pia Kuna
hatari ya kugongwa na magari kwasababu wanakatiza katika barabara kuu
itakayo Mwanza kwenda Bukoba.
Irene Rukia ambaye ni mjumbe wa
serikali ya mtaa wa Samina anasema kuwa maamuzi ya kujenga shule hiyo
yalifikiwa na wananchi ili kuweza kuwasaidia watoto wao kutembea umbali
mrefu pamoja na usalama wao kwasababu ya kuepuka ajali katika barabara
kuu.
Jimbo la Geita mjini ambalo kwa ujumla ndiyo Halmashauri ya
mji wa Geita ina jumla ya kata 13 na kwasasa mbunge wa Jimbo hilo ni
Constantine Kanyasu na Mwenyekiti wa Halmashauri ni Constantine Morandi
ambao wote kwa pamoja wanaahidi kwa kipindi Cha miaka 5 kushughulikia
kero za elimu, afya na maji.
Tags
Habari