Halima Mdee ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa wanawake jasri nchini Tanzania na Mbunge wa Viti Maalum amemchana 'live' mtu anayejihita Kigogo 2014 ingawa hakulitaja jina lake, lakini kutokana na mabandiko ya mara kwa mara ya huko Twitter huku yakimtuhumu Mdee na wenzake 18 ameamua kumkabili, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Wabunge wengine wa viti maalum ni Asia Mohamed, Felista Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Simon, Anatropia Theonest,Salome Makamba, Conchester Lwamraza, Grace Tendega, Ester Matiko,Secilia Pareso,Ester Bulaya, Agnes Kaiza, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga na Tunza.
Wabunge hao 19 waliosimamishwa uanachama na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hivi karibuni kupitia Mdee wameyasema hayo leo Desemba 1,2020 wakati wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.Halima Mdee amesema kuwa, wataendelea kuwa wanachama wa CHADEMA pasipo kujali yaliyotokea.
"Kama 2010, 2015 tulipinga matokeo ya uchaguzi, lakini bungeni tukaenda kwa nini 2020 tusiende labda kwa sababu ni wanawake," amesema Mbunge huyo wa Viti Maalum ambaye katika Bunge la 11 alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kawe aliloliongoza kwa vipindi viwili.
Mdee amesema, ameamua kuzungumza leo Desemba 1,2020 ili kutoa ufafanuzi kutokana na uongo unaoendelea kuzungumzwa na kusambaa mitandaoni.
“Nimekuja kuongea ili kutuliza haya mambo maana sio makubwa saaana, niliamua kukaa kimya ila naona uongo unasambazwa na ukiacha uongo uendelee kusemwa bila kutoa neno watu wataamini. Ieleweke kuwa, mimi ni mwana CHADEMA kwa miaka zaidi ya 16 sasa, nikiacha wazazi wangu, familia yangu ya pili ni CHADEMA, pamoja na kwamba mimi na wenzangu tumechukuliwa hatua za kinidhamu, niwahakikishie tu mimi na timu yangu tutabaki kuwa wana CHADEMA kindakindaki,"amesema Mdee.
Mdee amesema kuwa, kamwe thamani yake haiwezi kulinganishwa na fedha na kwamba, "wanaosema nimenunuliwa kwa Bilioni moja hakuna siri, walionipa watasema, hakuna yeyote aliyepewa hela. Huyo mtu ambaye simjui anayeandika sijui tumepewa ulinzi, hatujawahi kupewa ulinzi na Usalama wa Taifa wala Polisi. Nimemsoma huyo mtu nikiwa nyumbani Mbweni, mara anasema ooh! sijui tupo Masaki, kama analipwa na anatumwa kutuchonganisha na chama atasubiri sana kajitu kamoja sijui ni mtu wa aina gani? Sijui kama kamewahi kuitafutia CHADEMA hata mwanachama mmoja,"amesema."Mtu huyu siku hizi ndio amekuwa source wa taarifa za CHADEMA, inawezekana analipwa kutuvuruga, CHADEMA wanajua anawapa taarifa kumbe ana kamoja kaukweli, 99 ni uongo. Nitakuwa mwendawazimu kwamba jana nimewaonesha Uchaguzi ulivyoenda vibaya Kawe halafu leo nije kukubali kununuliwa, anayefikiria nimeishiwa imekula kwake,"amefafanu Mheshimiwa Mdee.
Pia amesema kuwa, kutokana na sintofahamu iliyojitokeza tarehe 26 Novemba 2020 walimuandikia barua Katibu Mkuu wakimuomba asogeze kikao mbele japo kwa wiki moja badala ya tarehe iliyokuwa imepangwa kwa wao kuitwa katika kikao husika wakihofia usalama wao" kutokana na uhamasishaji mkubwa uliokuwa ukifanywa na viongozi wetu wakubwa kwenye mitandao, ambao waliwaambia wanachama waje watushughulikie kwa kutupiga mawe kwa sababu ya usaliti wetu,"amedai.