Aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amekabidhi rasmi ofisi ya wizara hiyo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashinda Ndaki huku akijivunia mafanikio lukuki yaliyopatikana katika Sekta za Mifugo na Uvuvi katika kipindi alichoongoza wizara hiyo ikiwemo mapato ya sekta za wizara hiyo kuongezeka kwa mwaka kutoka wastani wa sh. bilioni 21 mwaka 2015 hadi kufikia sh bilioni 74 mwaka 2020 sawa na ongezeko la asilimia 252.4, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akimkabidhi ofisi Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki mji wa Serikali Mtumba. Kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul.
Akizungumza wakati akikabidhi ofisi kwa Waziri Ndaki, Mpina amrsema mafanikio hayo yaliyotokana na usimamizi thabiti na kuzuia ukwepaji wa mapato ya Serikali kupitia usimamizi operesheni na doria mbalimbali ikiwemo Operesheni Sangara, Operesheni Jodari na Operesheni Nzagamba.
Amesema, kupitia taasisi za TALIRI na TAFIRI, Serikali ilifanikiwa kuandaa Ajenda za Utafiti, Kanuni za utafiti, Kanzidata za Tafiti za Mifugo na Uvuvi ambapo zimepelekea kuongezeka kwa wigo wa kufanya utafiti, kufungua makabati yaliyohifadhi tafiti, kuweka misingi ya kisheria na kutoa mwongozo na wajibu wa majukumu kwa watafiti, kuorodhesha na kuweka tafiti zote pamoja, hali iliyopelekea kuongezeka kwa tafiti zilizoorodheshwa kufikia tafiti 933 mwaka 2020 ikilinganishwa na tafiti 33 zilizoorodheshwa mwaka 2015.
Aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akiagana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Mashimba Ndaki muda mfupi baada ya kukabidhi rasmi ofisi katika Mji wa Serikali Mtumba. Kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul na Katibu Mkuu Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah.
Ameongeza kuwa, wizara ilifanya mapitio ya Sheria na Kanuni na kuzifanyia marekebisho pamoja na kutunga Sheria na Kanuni mpya ili kurekebisha kasoro zilizokuwepo. Jumla ya Sheria na Kanuni zilizofanyiwa marekebisho ni 33 zikiwemo 27 za Sekta ya Mifugo na 6 za Sekta ya Uvuvi.
Amesema, marekebisho makubwa ya aina hii hayajawahi kutokea katika kipindi kingine chochote katika Wizara hiyo na hivyo kuondoa changamoto na kupunguza malalamiko ya wafugaji na wavuvi na hivyo kuongeza tija katika uzalishaji na biashara.
Mpina ameongeza kuwa, katika kipindi chake wizara ilianzisha Dawati la Sekta Binafsi ili kuwaunganisha wadau wa Sekta ya Mifugo na Uvuvi katika kupata huduma mbalimbali ikiwemo kuwaunganisha na Taasisi za Kifedha, bima na hifadhi za jamii, kushiriki utatuzi wa changamoto za kibiashara na uwekezaji kwa kuwaunganisha na taasisi na mamlaka nyingine za Serikali kama vile TRA, TBS, TMDA, Wizara, Halmashauri.
Pia Dawati limefanikisha upatikanaji wa mikopo katika Sekta za Mifugo na Uvuvi kufikia kiasi cha shilingi bilioni 64.2 mwaka 2020. Kipindi cha nyuma hapakuwepo na mikopo iliyotolewa na taasisi za fedha katika sekta hizo.
Aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akimkabidhi ofisi Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki mji wa Serikali Mtumba. Kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul.
Pia Serikali ilifanya tathmini ya kodi na tozo ambazo zinalalamikiwa na wadau, ambapo kupitia Muswada wa Sheria ya Fedha 2020 ilipelekea kufutwa kwa kodi nane (8) katika ununuzi wa vifaa na zana za Ukuzaji Viumbe Maji. Aidha, jumla ya tozo 85 za mifugo na uvuvi zimepunguzwa viwango katika mwaka 2020 na kuleta unafuu mkubwa kwa wadau.
Mpina amesema, kujengwa kwa viwanda vipya vya kimkakati ikiwemo TANCHOICE Company Limited kilichopo Kibaha Mkoa wa Pwani, Kiwanda cha ELIA FOOD OVERSEAS LIMITED Wilaya ya Longido Mkoa wa Arusha, Kiwanda cha BINJIANG COMPANY LIMITED – Shinyanga, Machinjio ya Kisasa ya Vingunguti. Viwanda hivi vinne (4) vya nyama vilivyogharimu jumla ya shilingi bilioni 83 vyenye uwezo wa kuchinja ng’ombe 5,500 na mbuzi/kondoo 14,000 kwa siku. Viwanda hivi vitawezesha Taifa kuuza nyama nje ya nchi kwa kiasi kikubwa kuliko ilivyo sasa, kutatua tatizo la ukosefu wa soko la mifugo ambapo hivi sasa hulazimika kuuza mifugo hai katika nchi jirani, kuongeza ajira kwa vijana na upatikanaji wa fedha za kigeni na kukuza uchumi wa nchi.
Kuhusu utatuzi wa migogoro ya wafugaji, wakulima na watumiaji wengine wa ardhi, Mpina alisema migogoro hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa matukio ya kupigana na kuuana baina ya wakulima na wafugaji, kulishwa sumu na kukatwa mapanga mifugo, ukamataji holela wa mifugo yamepungua kwa kiasi kikubwa tofauti na ilivyokuwa zamani kabla ya Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani.
Aidha Serikali iliongeza mapambano dhidi ya magonjwa yanasumbua mifugo ambapo majosho mapya 104 yamejengwa na majosho 542 yamekarabatiwa, kuanza kutolewa kwa dawa ya ruzuku ambapo majosho yote yanayofanya kazi yamepewa dawa ya ruzuku na kupelekea michovyo ya kuogesha mifugo kuongezeka kutoka michovyo 19,988,280 mwaka 2015/16 hadi michovyo 251,389,517 mwaka 2020 hali iliyopelekea maambukizi ya magonjwa kupungua kwa asilimia 29 na vifo vya mifugo kupungua kwa asilimia 37.
Hata hivyo kwa upande wa uvuvi amesema, mipango ya ujenzi wa bandari ya uvuvi iko hatua ya mwisho ambapo upembuzi yakinifu uko hatua za mwisho na mipango ya kupata fedha za mkopo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini kupitia ‘Exim Bank of Korea’ iko hatua za mwisho kwa ajili ya kupata fedha za ujenzi wa bandari hiyo.
Mpina katika kuanza uvuvi wa bahari kuu tayari Shirika la Uvuvi (TAFICO) limefufuliwa ambapo uandaaji wa Mpango Biashara (Business Plan) umekamilika, Serikali ipo katika hatua za mwisho ili kuingia mkataba na Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo Duniani (IFAD) kwa ajili ya kupata mkopo wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 68.8 ambazo zitatumika kununua meli za Uvuvi wa Bahari Kuu aina ya Longliner na Kujenga kiwanda cha Kuchakata samaki.
Amesema, mauzo ya samaki na mazao ya uvuvi nje ya nchi yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 379.25 mwaka 2015/2016 hadi shilingi bilioni 692 mwaka 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia 82.5 huku uagizaji samaki kutoka nje ya nchi ukipungua kutoka shilingi bilioni 56.12 mwaka 2016/2017 hadi shilingi bilioni 0.16 mwaka 2020 sawa na upungufu wa asilimia 99.7. Hivyo, kusaidia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni, kusaidia kulinda soko la ndani, kuongeza ajira na kupunguza ulali wa kibiashara.
Pia uzalishaji wa vifaranga vya samaki katika vitotoleshi vya Serikali na Sekta binafsi umeongezeka kutoka 8,090,000 mwaka 2015 hadi kufikia vifaranga zaidi ya 50,000,000 mwaka 2020. Kutokana na uzalishaji huo hivi sasa nchi yetu haiagizi tena vifaranga vya samaki kutoka nje ya nchi.
Aidha Mpina alisema operesheni Sangara, NMATT na Jodari zimeleta mafanikio makubwa ambapo jumla ya vipande 1,280,906 vya nyavu haramu vimekamatwa na kuteketezwa kwa moto; mabomu 4,583 yalikamatwa na watuhumiwa 14,384 walikamatwa na kutozwa faini na wengine kufikishwa mahakamani ambapo kumepelekea uvuvi na biashara haramu ya mazao ya uvuvi katika maji baridi kupungua kwa asilimia 80 na uvuvi haramu wa kutumia mabomu na milipuko mingine kupungua kwa asilimia 100 katika Mwambao wa Bahari ya Hindi.
Hivyo Mpina alimshukuru Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kuhudumu katika Serikali yake kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita ambapo alimuomba Waziri Ndaki kulinda mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano yaliyopatikana katika kipindi chake cha kwanza cha utawala wa Dk. Magufuli.
Kwa upande wake Waziri Ndaki amemhakikishia Mpina kuwa mafanikio yaliyotapikana katika kipindi chake atayaendeleza ili kuhakikisha sekta za mifugo na uvuvi zinakua na kutoa mchango mkubwa zaidi kwa taifa.
Pia Waziri Ndaki amemshukuru Mpina kwa namna alivyomkabidhi ofisi na nyaraka muhimu za kazi zilizofanyika awamu iliyopita ambazo zitamuongoza kujua aanzie wapi katika kutekeleza majukumu yake mapya ya kuwatumikia watanzania aliyokabidhiwa na Rais Dk. Magufuli
Tags
Uchumi