Zaidi ya watu 13 wameuawa katika milipuko miwili inayoripotiwa kuutikisa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Aden uliopo Kusini mwa Yemen huku mamia wakijeruhiwa, anaripoti Mwandishi Diramakini (Mashirika).
Hali ya tafurani ikiendelea baada ya mlipuko huo. (Picha na AP).
Tukio hilo la Desemba 30, 2020 limejiri muda mfupi tu baada ya kuwasili ndege iliyokuwa ina wasafirisha wajumbe wa serikali mpya ya umoja wa kitaifa.
Kwa mujibu wa mashirika ya habari za Kimataifa, katika tukio hilo hakuna kati ya maafisa hao wa serikali waliojeruhiwa, lakini inaripotiwa watu wengi wamejeruhiwa na huenda idadi ya vifo ikaongezeka.
Aidha, haijafahamika mara moja kilichosababisha milipuko hiyo, lakini milio ya bunduki ya hapa na pale ilisikika karibu na uwanja huo.
Serikali ya Yemen inayotambulika kimataifa na wapiganaji wanaotaka kujitenga huko Kusini wameunda serikali mpya ya pamoja kushirikiana madaraka, hatua iliyochukuliwa Disemba 18 na waliwasili katika mji huo wa Kusini wa Aden Jumatano baada ya kuapishwa nchini Saudi Arabia.
Serikali hiyo ya wajumbe 24 iliundwa chini ya usimamizi wa serikali ya Riyadh ambayo inaongoza muungano wa nchi za Kiarabu unaopambana na Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran wanaoshikilia mji mkuu wa Sanaa tangu mwaka 2014.
Serikali hiyo mpya iliyoapishwa na Rais Abderabbo Mansour siku ya Jumamosi imeundwa kupambana na uasi unaoendelea katika sehemu kubwa ya Kaskazini mwa nchi.