Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Inades Formation Tanzania (IFT) inatekeleza shughuli zake kwa lengo la kuchangia jitihada za serikali katika kuleta maendeleo pamoja na maisha bora kwa wananchi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
IFT hupata ufadhili wa shughuli zake kutoka kwa washirika mbalimbali wa ndani pamoja na wa nje ya nchi na kwa muda mrefu uhai wa taasisi umebebwa na wahisani au kwa wafadhili kutoka Ujerumani kupitia Bread for the World.
Wahisani hao wamekuwa wakifadhili miradi kwa miaka takribani zaidi ya 15 na bado wanaendelea kushirikiana nao katika kutekeleza miradi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Walengwa wakuu wa mradi huu ni wakulima wadogo wanaoishi kwenye maeneo ya vijijini wanaojihusisha na ufugaji wa mnyama punda.
Taasisi hiyo ndiyo inayosimamia mradi wa mnyama punda kwa lengo la kusaidia maisha ya jamii za vijijini kukuza ustawi wa mnyama punda –Brooke East Africa –Kenya kupitia Brooke UK.
Mradi wa mnyama punda ni matokeo ya utafiti uliofanyika mwaka 2017 mkoani Singida na mkoani Iringa kuhusu mnyama punda na kwamba matokeo ya utafiti huo yalionesha kwamba mnyama punda ana mchango wa moja kwa moja katika maisha ya watu.
Katika makala haya baadhi ya akina mama wa Kijiji cha Endesh,Kata ya Merya Wilaya ya Singida wanazungumzia faida za mnyama punda jinsi walivyowapunguzia kazi,kuwaongezea kipato na kuokoa rasilimali fedha pamoja na muda kwa kumtumia mnyama punda.
Restuta Musa ni mkazi wa Kijiji cha Endesh anasema, punda ni mnyama mzuri na anawasaidia sana kwa baadhi ya kazi kama vile kuchota maji,kulima pamoja na kubebea kuni.
Mwasiti Athumani mkazi wa Kijiji cha Endesh anasema kwamba, yeye ni mmoja wa wafugaji wa mnyama punda na kila inapofika tarehe ya maadhimisho ya siku ya punda duniani humpumzisha punda wake kufanyakazi ambazo humsaidia kwa siku za kawaida.
Anafafanua mkazi huyo kuwa kutokana na juhudi alizonazo mnyama huyo za kujituma kufanyakazi kwa bidii humtunza kwa kumpatia chakula cha kutosha na maji safi na salama ya kutosha.
Naye Juliana Salimu mkazi wa Kijiji cha Endesh anasema, tangu Taasisi ya Inades Formation Tanzania ilipoanza katika kijiji hicho iliwafundisha matunda ya punda,walikuwa hawajui namna ya kumtunza mnyama huyo lakini hivi sasa wamejua.
Winfrida Stephano ni mkazi wa Kijiji cha Endesh anasema, amekuwa akimtumia mnyama punda kumbebea mizigo yake kupeleka sokoni,ambayo inampatia kipato cha fedha na fedha zinazopatikana huwekwa kwenye vikoba na kugharamia masomo ya watoto wake.
Akiongea katika mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Singida,Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Elia Digha anaiomba serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuangalia uwezekano wa kutunga sheria itakayomlinda mnyama punda kutouzwa popote pale ili awe sawa na wanyama wengine,akiwemo tembo ambaye serikali imepiga marufuku mnyama huyo kuuawa.
Digha ambaye pia ni diwani wa Kata ya Msange anaongoza uchangiaji wa mada iliyotolewa na Mkufunzi wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la Inades Tanzania,lenye makao yake mkoani Dodoma,Grace Mketto.
Mwenyekiti huyo anasisitiza kuwa haitawezekana wananchi wa Halmashauri hiyo kuishi bila kuwepo kwa mnyama punda au kitu chochote ambacho kinawasaidia wananchi wao,kwa hali hiyo umefika wakati sasa kwa wanyama wa aina hiyo kuingizwa katika utaratibu wa kulindwa kisheria.
“Punda sisi tunaamini siku zote ni mnyama anayetusaidia,sasa punda wanauzwa nchi inaangalia karibu wote wanaisha,kwa nini viwanda vinajengwa kwa ajili ya punda wetu tu wakachinjwe mbona punda wale weusi wa wachina wao hawawachinji,wanataka kutuletea sisi,”anahoji Digha ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Msange.
Hata hivyo Digha anasisitiza pia kwamba uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Singida hautakuwa tayari kupokea punda wale weusi kutoka kwa wachina,kwa kuwa wanawaamini punda wao kwani hawaugui ovyo ovyo na uzazi wa punda ni wa muda mrefu sana.
“Tunashangaa viwanda vinajengwa kwa ajili ya kuchinja punda wetu,mbona punda wao weusi hawawachinji ili watuletee punda wao weusi punda wetu anajiamini na hawaugui na uzazi wake ni wa muda mrefu kweli kweli peleka ule ujumbe mara moja,”anaweka bayana msimamo wa Halmashauri.
Vile vile Digha anaonyesha kukerwa sana na maamuzi ya kuchinjwa kwa punda licha ya kuwepo kwa serikali,kupitia wizara ya mifugo na uvuvi,lakini mnyama punda anakwenda kuchinjwa na wachina na kuna siku wakaambiwa wanachinjwa ili wabadilishwe mfumo na kupatiwa punda mweusi.
“Kwa nini punda weusi wasiwale wao,halafu sisi tuendelee kuishi na wa kwetu ambao hatuna shida,wao wanataka punda wetu wawachinje wakwao weusi hawawachinji,”anasisitiza mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya wilaya ya Singida.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo anaonekana kupigwa na butwaa kutokana na uamuzi wa wizara unaoruhusu punda weusi wahamishwe na kuletwa nchini wakati watanzania wana punda wao ambao wamewafanya kuwa wanyamakazi wa kulima,kuchota maji na kubeba mizigo.
Akiwasilisha mada kuhusu matumizi ya mnyama punda,Mkufunzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Inades Tanzania lenye makao yake mkoani Dodoma,Grace Mketto anasema shirika hilo kwa kushirikiana na wizara wapo kwenye mchakato wa kuhakikisha kwamba wanatetea ustawi wa punda.
Hata hivyo mkufunzi huyo anafafanua pia kuwa pamoja na kutetea ustawi wa mnyama huyo,lakini pia wana kampeni ya kuhakikisha kwamba punda wa Tanzania haibiwi,hatoroshwi na wala hachinjwi kutokana na manufaa yake aliyonayo.
“Kwa hiyo niseme kwamba kwenye mkutano huu tunashirikiana kwa karibu sana na wizara ya mifugo na uvuvi na mwisho wa siku tutakuwa na mikakati madhubuti ya kutetea ustawi wa punda,”anasisitiza Grace
Wakichangia mada hiyo baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo,Iddi Kijida anaweka wazi kwamba kabla ya Halmashauri ya wilaya ya Singida haijatenganishwa na Halmashauri ya wilaya ya Ikungi punda walikuwa wakichinjwa katika Kijiji cha Damankiya,ndipo walipoamua kutunga sheria ndogo za kumlinda mnyama huyo.
“Sasa Mwenyekiti serikali zetu hizi za mitaa tuzijenge vizuri,kwani hawa wachina walipoingia sheria yetu ilitupwa wapi si wangekuja tu kwenye Halmashauri yetu jambo lolote linalotoka kule juu tuje huku chini tuanze pamoja mambo yatakuwa yanaenda vizuri,”anahoji Diwani huyo.
Kwa mujibu wa Iddi ambaye pia ni diwani wa Kata ya Merya na Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya huduma za jamii iwapo itaonekana punda wamekuwa wengi tutakubaliana kwa pamoja kuwauza au tuwale.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Singida,Rashidi Mandoa anasema Halmashauri ya wilaya ya Singida ina jumla ya aina 11 za wanyama wafugwao ambao ni pamoja na ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, kuku, bata, kanga,njiwa,mbwa,punda na paka.
Mandoa mwenye dhamana ya kusimamia shughuli mbali mbali za maendeleo katika Halmashauri hiyo anafafanua kwamba Halmashauri hiyo ina jumla ya ng’ombe 178,426,mbuzi 73,359,kondoo 41,183, nguruwe 373, kuku 371,878, bata 1,371, kanga 4,372, njiwa 3,916, mbwa 14,659 na paka 4,305.
Anasema utafiti wa mradi wa kuhusu mnyama punda ktika mikoa ya Singida na Iringa na matokeo ya utafiti huo uligundua kwamba mnyama punda ana mchango mkubwa kiuchumi na kijamii kwa wamiliki na watumiajiwa mnyama punda kwa kuwapatia kipato cha moja kwa moja wanapokodishwa kufanyakazi.
Lakini pia kipato ambacho si cha moja kwa moja wanapofanyakazi mbalimbali katika jamii ya wafugaji ambapo mradi huu umesaidia kuboresha maisha ya wanajamii kupitia matumizi sahihi ya punda kwa kuzingatia haki zake tano za msingi ambazo ni pamoja na kupewa chakula na maji ya kutosha,kutokuogopeshwa,kutokufanyishwa kazi zaidi ya uwezo wake,kutoumizwa na au kutojeruhiwa lakini pia kupewa matibabu anapougua na haki ya kuishi tabia yake ya asili.
Kuhusu sheria ndogo za kumlinda na kutetea haki za mnyama,Mandoa anabainisha kuwa Halmashauri hiyo imetunga sheria ndogo zinazomlinda na kutetea hakiza wanyama inayosema kila mnyama afugwaye anastahili kupewa huduma zote muhimu kama vile kupatiwa chakula na maji ya kutosha.
Nyingine kwa mujibu wa Mandoa ni haki ya kutokuogopeshwa,kutokufanyishwa kazi zaidi ya uwezo wake,kutoumizwa na au kutojeruhiwa lakini pia kupewa matibabu anapougua pamoja na haki ya kuishi tabia yake ya asili na kwamba sheria hiyo inamlenga zaidi mnyama punda.
Kuhusu mchango wa mnyama punda katika pato la kata,tarafa,wilaya,mkoa na taifa kwa ujumla,Mkurugenzi huyo anaweka wazi kuwa punda ni mnyama kazi na hufanyakazi mbali mbali za uzalishaji mali hasa shughuli za kilimo na usafirishaji wa mizigo.
“Punda ni mnyama kazi anafanyakazi mbali mbali za uzalishaji mali hasa shughuli za kilimo na usafirishaji wa mizigo na shughuli zote hizo ni chanzo cha kipato cha familia,Kijiji,Kata,Tarafa hadi Taifa.”anasisitiza Mandoa.
Hata hivyo Mandoa anatoa wito kwa wamiliki wa mnyama punda kutambua haki na sheria ili kuacha ukatili dhidi ya mnyama punda pamoja na pia kutambua mchango mkubwa wa punda katika maisha ya jamii na wafugaji wa punda wasirubunike kuuza punda kwani thamani ya haraka inaonyesha faida kubwa hupatikana kwa kumtumia punda kuliko kumuuza.
Naye Ofisa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya wilaya ya Singida,Theophil Ishengoma anasema Inades Formation Tanzania ni Shirika lisilo la kiserikali (NGO) ambalo linatoa elimu kwa jamii ya wakulima na wafugaji waishio vijijini namna ya kutambua thamani ya raslimali zinazowazunguka na kuzitumia kuboresha hali yao ya maisha.
Aidha Ishengoma anavitaja vijiji vya kwanza kunufaika na mradi huo kuwa ni pamoja na Endesh na Ghata na kwamba hata hivyo vijiji vya Sagara,Mjughuda,Maghojoa,Kinyamwenda na Mwasauya vimeanza maandalizi ya kutekeleza mradi wa uendelezaji wa mnyama punda.
Ishengoma anasema kuna vikundi nane ambapo kila Kijiji kina vikundi vinne vya wamiliki na watumiaji wa punda na kuyataja manufaa ya vikundi hivyo kuwa ni pamoja na kupatiwa elimu ya ufugaji bora wa punda na mifugo mingine na kuwezeshwa kuanzisha shughuli za akiba na mikopo.
Faida zingine ni kupatiwa elimu ya ujasiriamali ili kuweza kutumia raslimali na fursa zinazowazunguka kwa kuanzisha biashara ndogo ndogo,kupewa elimu juu ya masuala mtambuka kama vile jinsia na Ukimwi kupitia umoja wao na kwa mwaka 2020/2021 Inades Formation Tanzania inategemea kuviongezea mitaji vikundi vitakavyobuni na kuanzisha miradi yenye kusaidia kuongeza kipato cha wana kikundi wakati huo huo ikisaidia kuboresha ustawi a punda.
Ofisa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi anasema hakuna mapato ya moja kwa moja yanayoingia Halmashauri ya wilaya kutoka kwa punda bali kutokana na kazi zinazofanywa na mnyama punda Halmashauri inapata mapato yake kupitia ushuru hasa wa mazao ya kilimo.
Faida za mradi huo kwa siku za baadaye kwa mujibu wa Ishengoma ni kujenga uelewa juu ya umuhimu wa punda kwa jamii na kufanya jamii kutambua kuwa thamani ya punda hai ni kubwa kuliko pesa ipatikanayo kwa kumuuza na kumchinja hivyo kusaidia kutotoweka kwa mnyama huyo.
Anasisitiza kuwa Inades imejenga umoja imara wa wafugaji,watumiaji na wadau wengine kupitia vikundi na jukwaa la punda ambalo litaendelea kutoa mchango katika kuendeleza sekta ndogo ya punda katika Halmashauri nje ya Halmashauri.
Mradi umesaidia utungwaji wa sheria ndogo inayosaidia matumizi endelevu ya punda katika Halmashauri ya wilaya ya Singida kwa kuzingatia haki tano muhimu za wanyama.
Ofisa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi anabainisha idadi ya aina za mifugo zilizopo katika Halmashauri ya wilaya ya Singida kuwa ni ng’ombe178,426,mbuzi 73,359,kondoo 41,183,nguruwe 373,kuku 371,878,bata 1,371,kanga 4,372,njiwa 3,916,mbwa 14,659,punda 3,765 na paka 4,305.
Tags
Makala