Tariq Machibya (29) ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Mr. Kuku Farmer LTD maarufu Mr Kuku ameachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kukamilisha taratibu za kulipa faini ya shilingi milioni 5 alizotakiwa kulipa na mahakama hiyo, kutokana na kupatikana na hatia ya kosa la biashara ya upatu, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Machibya amelipa faini hiyo leo Desemba 17, 2020 kufuatia hukumu iliyotolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Issaya baada ya kukiri makosa na kuingia makubaliano ya kumaliza kesi hiyo kwa njia ya majadiliano baina yake na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Katika hukumu hiyo, Mahakama imemuhukumu mshtakiwa kulipa faini ya sh.milioni tano au akishindwa atatumikia kifungo cha miaka 10 gerezani katika makosa mawili aliyokutwa na hatia kati ya mashtaka saba yaliyokuwa yakimkabili awali kabla ya kuingia makubaliano na DPP.
Pia, mahakama iliamuru sh.5,456,480.41 ambazo zipo katika akaunti za mshtakiwa zitaifishwe na kuwa mali ya Serikali. Aidha, Mahakama iliamuru fedha hizo kuhamishiwa katika akaunti namba 9921169817 iliyoko Benki Kuu ya Tanzania kwa jina la Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).
Machibya aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kufanya biashara haramu ya upatu na kukusanya fedha za umma sh.Bilioni 17, ambapo amehukumiwa kulipa fidia ya zaidi ya sh. Bilioni 5.4 baada ya kukiri mashtaka ya kushiriki katika kosa hilo la upatu.
Wakati akisoma hukumu hiyo, Hakimu Issaya alisema amezingatia kwamba mshtakiwa amekiri mwenyewe makosa yake na ni mkosaji wa mara ya kwanza na wameangalia makubaliano hivyo hakuna sababu ya kumpa adhabu kali
Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa mshtakiwa pamoja na DPP wameingia makubaliano katika mashtaka saba aliyokuwa anakabiliwa nayo yameondolewa na wamebakisha mashtaka mawili
Akisomewa mashtaka hayo mawili, katika shtaka la kusimamia biashara ya upatu inadaiwa kati ya Januari 2018 na Mei, mwaka huu, maeneo tofauti jijini Dar es Salaam alijihusisha na biashara hiyo kwa kukubali na kukusanya fedha kutoka kwa umma kwa kujifanya watafanya ujasiriamali wa ufugaji kuku na watapata faida asilimia 70 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa miezi minne na asilimia 90 ya mtaji wa uwekezaji wa miezi sita kiasi ambacho ni kikubwa kibiashara kuliko mtaji uliokusanywa.
Katika shtaka la pili mshtakiwa anadaiwa kukubali kupokea muamala wa kifedha kutoka kwa umma kiasi cha sh. bilioni 17.Awali, mshtakiwa alikuwa anakabiliwa na mashtaka saba ambapo mbali na hayo mawili yalikuwepo mashtaka matano ya utakatishaji fedha huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Tags
Mahakamani