Wakiwa uwanja wa nyumbani timu ya Mtibwa Sugar leo Desemba 11, 2020 imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Bao pekee la ushindi limepachikwa na Salum Kihimbwa dakika ya 21 kwa kichwa akimalizia pasi ya Kanoni.
Aidha, licha ya jitihada za KMC FC kupambana kupitia nyota wao Relliants Lusajo na Emmanuel Mvuyekure kupata bao la kusawazisha milango ilikuwa migumu.
Kihimbwa amesema kuwa, walipata nafasi nyingi kwenye mchezo huo ila walishindwa kuzitumia licha ya kupata alama tatu muhimu.
Aidha, Juma Kaseja, nahodha wa KMC FC ambaye ni kipa namba moja amesema kuwa, makosa ambayo wamefanya yamewaponza wapoteze alama tatu kwenye mchezo huo.
Hata hivyo, kwa ushindi huo, Mtibwa Sugar inafikisha pointi 19 baada ya kucheza mechi 15 na kupanda nafasi ya tisa kutoka ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakati KMC inayobaki na pointi zake 21za mechi 13 sasa inabaki nafasi ya tano katika msimamo huo.
Tags
Michezo