NMB kushirikiana na Serikali ya Zanzibar kukuza utalii

Benki ya NMB imesema kuwa imejipanga na kukusudia kuhakikisha inashirikiana na serikali katika kuona sekta ya utalii inakidhi mahitaji ya uchumi wa taifa ikiwa ni pamoja na kukuza Sekta ya Utalii ambayo imekuwa tegemeo kubwa la uchumi Zanzibar, anaripoti Mwandishi Diramakini (Zanzibar).
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdalla akimkabidhi cheti Mkuu wa Idara ya Biashara za Kadi wa Benki ya NMB, Philbert Casmir ikiwa ni utambuzi wa benki kwa kushiriki Mkutano wa Jumuiya ya Makampuni ya Waongoza Watalii Zanzibar. NMB ilidhamini mkutano mkuu wa mwaka.

Benki hiyo imebainisha kuwa na mtaji wa kutosha na imejitolea kutumia wataalamu wake kuona mfumo wa uendeshaji wa Sekta ya Utalii kupitia Teknolojia ya kisasa ya Mawasiliano unakwenda kwa kasi na kuleta matumaini makubwa hasa visiwani Zanzibar.

Hayo yamesemwa na Meneja Mwandamizi Biashara na Serikali wa NMB, Adelard Mang'ombo katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Makampuni ya waongoza misafara ya Watalii Zanzibar (ZATO) uliofanyika Zanzibar.
Meneja Mwandamizi Biashara za Serikali wa Benki ya NMB , Adelard Mang'ombo akizungumza wakati wa Mkutano wa Jumuiya ya Makampuni ya Waongoza Watalii Zanzibar. NMB ilidhamini mkutano mkuu wa mwaka.

Adelard amesema kuwa, NMB inatambua kuwa uchumi wa Zanzibar unategemea sana shughuli za utalii, ambapo kama Benki kubwa nchini imejipanga kuhakikisha uchumi huo unaendelea kukua na kuwaletea wazazibar maendeleo.

“ Benki yetu ina mtaji mkubwa, kupitia mafanikio haya, tunaona kuna umuhimu wa kuungana na Serikali na tumekusudia katika hilo, kuhakikisha tunashiriki na sisi katika kukuza uchumi wa nchi kupitia Sekta ya Utalii,”amesema Mang’ombo.
Maafisa wa Benki ya NMB Tawi la Zanzibar, wakimwelezea Kamishna wa Uhamiaji, Jecha Makame Issa kuhusu bidhaa na huduma za benki hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Biashara za Kadi Benki ya NMB, Philbert Casmir amesema, NMB imekusudia kutoa ushirikiano mkubwa kwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuhakikisha inasaidia kukusanya mapato na kujenga uchumi.

Amesema, benki hiyo inaamini kuwa uwezo wake katika kukusanya mapato yanayohusu Sekta ya Utalii, itasaidia kwa kiasi kikubwa kukusanya mapato na kupelekea kufikia lengo la uchumi wa buluu.
Meneja Mwandamizi wa Biashara za Serikali wa Benki ya NMB, Adelard Mang'ombo (kushoto) na Meneja Mahusiano Biashara za Serikali wa Benki ya NMB, Mkunde Joseph (kulia) wakibadilishana mawazo na Mkurugenzi wa Mipango Wizara Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapindizi Zanzibar, Abdullah Issa Mgongo.

Kuhusu uchumi wa buluu, Casmir amesema kuwa, Benki ya NMB imejipanga kushirikiana na serikali kutimiza maono yake kwenye uchumi wa bluu na tayari wameanza kwa vitendo kwa kuzindua jukwaa la biashara linalowezesha wafanyabiashara kufanya miamala kupitia tovuti zao (E-Commerce Platform).
Mkuu wa Idara Biashara za Kadi wa NMB, Philbert Casmir (mwenye koti) akizungumza na wadau wa Jumuiya ya Makampuni ya Waongoza Watalii Zanzibar, pamoja naye ni Meneja Mahusiano wa Biashara za Serikali wa NMB,Mkunde Joseph.

Aidha, amesema kuwa, wamewezesha matumizi ya kadi za malipo za UnionPay na sasa inakubalika katika kufanyia miamala kwenye mashine za kutolea fedha (ATM) na zile za kufanyia manunuzi (POS) za NMB, lengo likiwa kuleta huduma bora kwa wafanyabiashara waliopo kwenye Sekta ya Utalii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news