Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya, amekitaka Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kutangaza huduma zinazotolewa kituoni hapo ikiwemo mafunzo ya uongezaji thamani madini yanayotolewa ili kukiwezesha kukua na kutambulika kwa wadau wengi zaidi wa ndani na nje ya nchi, wanaripoti Asteria Muhozya na Steven Nyamiti (WM) Arusha.

Aidha,
amesisitiza kituo hicho kutumia vyombo vya habari kujitangaza kwa lengo
la kuwezesha mafunzo na huduma zake kutambulika zaidi kwa walio wengi
suala ambalo litawezesha azima ya Serikali kuchochea shughuli za
uongezaji thamani nchini kufanikiwa.

Ameongeza kuwa, kituo hicho kinayo maabara ya kupima madini ya vito, hivyo, hakuna haja ya watanzania kudanganywa kwani ipo sehemu ambayo wanaweza kupata huduma ya kutambua madini halisi na yaliyotengenezwa.
Katika hatua nyingine Prof. Manya amekipongeza Kituo cha TGC kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi katika fani ya ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito, fani ya usonara, fani ya uchongaji wa vinyago vya vito, utambuzi wa Madini ya Vito na Utengenezaji wa bidhaa za mapambo na urembo na kueleza kuwa, mafunzo hayo yanalenga katika kuongeza tija kwenye sekta ya madini ikiwemo kutoa nafasi ya ajira kwa watanzania ikiwemo kujiajiri.
Kituo cha TGC kipo jijini Arusha, kwa mujibu wa Mratibu wa Kituo hicho, vijana wengi ambao wamehitimu katika kituo hicho wamepata nafasi ya kuajiriwa katika kampuni zinazofanya shughuli za uongezaji thamani jijini humo kutokana na kuwa na ujuzi wa kiwango cha juu.
Tags
Habari